Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, imeipongeza Wizara ya Maji kwa utekelezaji wa mradi wa maji wa Itagutwa ambao unahudumiwa jumla ya wananchi 1645 wa Kijiji cha Itagutwa.

Pongezi hizo zimetolewa leo Machi 13, 2024 Mkoani Iringa, baada ya Kamati hiyo kutembelea mradi, ambapo imejionea kazi zilizofanyika zikiwemo za ulazaji mabomba wa umbali wa kilometa 12.75 , Ujenzi wa vituo 11 vya kuchotea maji pamoja na ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita elf 75.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jackson Kiswaga amesema utekelezaji wa mardi huo, utasaidia kutatua changamoto ya maji kwenye Kijiji cha Itagutwa pamoja na baadhi ya vitongoji vilivyopo kwenye vijiji vya Jirani.

Akiwasilisha taarifa ya Mradi Meneja wa RUWASA Wilaya ya Iringa, Mhandisi Exaud Humbo ameelezea kuwa kuwepo kwa mradi huo kutaongeza shughuli za uzalishaji kwa kuokoa muda wa wananchi waliokuwa wakiutumia kutafuta maji.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Maji, Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema Wizara inaendelea na jitihada ili kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi wote.

Aidha, Mahundi amemuagiza Meneja wa RUWASA wa Wilaya ya Iringa Mhandisi Exaud Humbo kuhakikisha anasimamia vijiji vya kipengele na Mapululu viweze kujengewa vituo sita vya kuchotea maji, huku vijiji viwili ikiwemo Kijiji cha Kipengele vijengewe vituo vitatu vya kuchotea maji na mpaka kufikia tarehe 30 Aprili, 2024 viwe vimekamilika.

Mradi wa maji wa Itagutwa, ulisainiwa Januari 16, 2023 na utekelezaji wake ulianza Mei 10,  2023 ukiwa na gharama ya mradi ya shilingi milioni 322.

 

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Machi 14, 2024
Makamba: Rwanda kujenga Kiwanda cha Maziwa Mwanza