Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’, Wallace Karia, amesema vifaa vya kiteknolojia kwa ajili ya kuwasaidia waamuzi ‘VAR’, vitaanza kutumika rasmi katika mechi za Ligi Kuu Bara kuanzia msimu ujao.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Karia amesema tayari wameshapokea nyaraka kutoka katika Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’, kwa ajili ya kupokea vifaa vya VAR, lakini kabla ya hapo kutakuwa na mafunzo kwa waamuzi ya namna ya kuvitumia.

“Ndiyo, tayari CAF wametusaidia wanatuletea VAR katika ule mpango wake wa kusaidia ‘zone’zake, lakini kwanza kutakuwa na mafunzo ya jinsi ya kuitumia, tumeshapokea nyaraka, na tuko katika mchakato wa kuomba kusamehewa kodi serikalini kabla kupokea ule mzigo wenyewe wa vifaa kabla ya mbali na VAR itakayoletwa kwa msaada wa CAF kufungwa,” amesema Karia.

Amesema wadhamini wao waliochukua jukumu la kuonyesha mpira kwenye televisheni nao wamemwahidi kununua mashine inayotembea, hivyo Tanzania kutakuwa na VAR mbili, ingawa amesema inabidi kanuni za ligi zirekebishwe kwani baadhi ya mechi zitakuwa zinachezwa bila kifaa hicho.

Rais huyo amesema VAR inayotembea itaanza kufanyiwa majaribio katika mashindano ya Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati ‘CECAFA’ yatakayofanyika kuanzia Juni 29 hadi Julai 14, mwaka huu huko Zanzibar.

“Wadhamini wetu wanaoonyesha mpira kwenye televisheni nao wamesema watanunua VAR inayotembea, yenyewe itakuwa inahamishika, inaweza kuwa uwanja huu leo, kesho ikaenda kutumika kwenye Uwanja mwingine, ile ya CAF yenyewe itafungwa kwenye Uwanja wa Mkapa, kwa hiyo itatumika hapo, tuna hii ya kuhamishika itakwenda Tanga au Morogoro,” Karia amesema

Ameongeza lazima zitengenezwe kanuni kwa sababu haiwezekani katika mechi nane, ni michezo mwili tu ndiyo iwe na VAR na mechi nyingine zichezwe kavu.

Ameeleza kanuni zitakazotungwa ndizo zitatoa mwongozo kwa VAR hizo mbili zitumike vipi, lakini kwa anavyoona kwa kiasi kikubwa zinaweza kutumika katika michezo inayohusu Simba SC na Young Africans pale zinapokuwa kwenye viwanja viwili tofauti.

“Mara nyingi mechi zinazotusumbua ni zile ambazo wanacheza hawa wakubwa (Simba SC na Young Africans), wanashindana wenyewe, kila mmoja anaweka watu wake kwa ajili ya kurekodi makosa ya waamuzi yanayomnufaisha mwenzake na kurusha, huwezi kuona mechi ya Coastal na Ihefu makosa ya waamuzi yanarushwa na kujadiliwa katika mitandao ya kijami,” ameongeza Karia.

Amesema imefika wakati wa kuwalinda waamuzi wa Kitanzania ambao wanaheshima katika mashindano ya kimataifa yanayosimamiwa na CAF kwa kuwaletea VAR.

“Wenzetu wanawalinda sana marefa wao, Wanafanya mambo ya ajabu sana, Waamuzi ni binadamu, wengine wanapitiwa, wengine wanafanya makusudi, lakini wanalindwa, pia wanasaidia wa VAR, kwetu likifanyika tu tunawarushia dunia nzima,” amesema kiongozi huyo

Balozi Shelukindo aongoza ujumbe wa Tanzania Mkutano SADC Zambia
Polisi yatoa tahadhari urafiki wa Mtandaoni