Wakati Simba SC ikiingia chimbo visiwani Zanzibar kuweka kambi fupi ya maandalizi ya mechi za Hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya AI Ahly Machi 29, wenzao wameanza kuingiwa hofu juu ya mchezo huo.

Kiungo wa Waarabu hao ambao msimu uliopita kwenye ligi ya ndani walipoteza mchezo mmoja, Alou Dieng amekiri kama kuna kitu kinachemsha akili zao kwa sasa ni umuhimu wa mechi hiyo ya Dar es salaam.

Simba SC itakutana na Ahly, klabu inayoongoza kwa kutwaa mataji mengi Afrika kwenye mechi mbili za hatua ya Robo Fainali na mechi ya kwanza itapigwa ljumaa (Machi 29) Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam na kurudiana wiki moja baadae jijini Cairo, Misri Aprili 5.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Cairo, Alou Dieng amesema hana uhakika kama ataziwahi mechi hizo kutokana na majeraha yake, lakini anaamini itakuwa Robo Fainali ngumu akionyesha mambo manne yanayoweza kuwasumbua.

Dieng raia wa Mali amesema ingawa wana uhakika wa kuwang’oa Simba SC lakini wasiwasi wao wa kwanza ni Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambao muda mrefu wameshindwa kutoka na ushindi na sasa wanakuja kwenye kipindi ambacho Mnyama anataka kufuzu.

Pia kiungo huyo ambaye amekulia kwenye akademi moja na Mlinda Lango wa Young Africans Djigui Diarra, amesema Simba SC ya sasa ina wachezaji wakomavu wanaojua kucheza na kuamua mechi kubwa tofauti na awali.

Ameongeza pia uwepo wa kocha wa sasa, Abdelhak Benchikha kutazifanya mechi hizo kuwa ngumu kwavile ana uzoefu na michuano hiyo na anakuwa na malengo ya kufika mbali kwa kuangalia rekodi zake za timu za Arabuni alikopita.

Amesisitiza pia hata matokeo ya hivi karibuni kwenye michuano ya AFL yatachagiza mchezo huo, kwani Simba SC imebadilika na inaweza kufanya chochote, ingawa wao wanataka kupata matokeo Dar es salaam kisha wakamalizane Cairo ambako wanawamudu zaidi Simba SC.

“Sina uhakika wa kuziwahi hizo mechi ndio naanza kupona taratibu lakini naiamini timu yangu itawang’oa Simba SC, tuna timu bora Afrika hii,” amesema Dieng

“Al Ahly Tunajua tunakutana na Simba SC moja ya klabu bora Afrika, wana wachezaji wenye uzoefu mkubwa tutawatoa lakini wasiwasi wangu ni mechi ya Tanzania ambapo tumeshindwa mara kadhaa kuondoka na ushindi pale matokeo ya mechi hiyo kama hayatakuwa mabaya kwetu tutawaondoa kirahisi.”

“Ukikiona kikosi chao halafu akaongezeka na huyu kocha kutoka Algeria (Benchikha) unaona jinsi ugumu utakavyokuwa, huyu ni kocha ambaye alitusumbua mara ya mwisho tulipokutana naye, lakini kwa namna yoyote wakija kwetu tutawamaliza,” anasema Dieng ambaye ni miongoni mwa mihimili ya timu hiyo.

Ameeleza anajivunia kuimarika kwa kiwango cha timu yake kwa sasa hasa eneo la ushambuliaji ambalo lilikuwa halijafanya vizuri sana katika miezi ya hivi karibuni kwenye michuano mbalimbali.

“Timu yetu sasa imeimarika zaidi tofauti na huko nyuma wakati tulipokutana nao (Simba SC) tunaweza kufunga uwanja wowote sasa, tutafanya vizuri na kutinga Nusu Fainali na kwenda kutetea ubingwa wetu.”

Mara ya mwisho Simba SC kukutana na Al Ahly ilikuwa katika AFL kutoka na sare 2-2 kwa Mkapa na 1-1 Cairo na Al Ahly kuwatoa Wekundu hao kwa kanuni ya bao la ugenini.

Katika miaka ya hivi karibuni timu hizo zimekuwa na uswahiba mkubwa nje ya uwanja na mara kadhaa Simba SC imewahi kutembelea miundombinu ya Al Ahly kwa ajili ya kujifunza mafanikio yao nje na ndani ya uwanja.

Al Ahly kocha wao ni Mswisi, Marcel Martin Koller ambaye amewahi kufundisha Bundesliga kwa misimu kadhaa na Uswisi. Wametwaa makombe 11 ya Ligi ya Mabingwa na ndio mabingwa watetezi kwa sasa.

Msimu uliopita Ahly iliwatoa Raja Casablanca ya Morocco kwa jumla ya mabao 2-0 na kufuzu Nusu Fainali walikomtoa Esperance ya Tunisia kwa mabao 4-0 na kwenda Fainali walikowapiga Waydad mabao 3-2 na kubeba ubingwa wao wa 11.

Dkt. Mzuri awasilisha shukrani uwezeshaji Wanawake kudai haki Kidemokrasia
Bayern Munich kutupa karata ya mwisho