Kocha Mkuu wa Geita Gold, Denis Kitambi, amewashukia wachezaji wake ambao amedai walicheza kwa dharau dhidi ya timu ya Daraja la Pili, Rhino Rangers na kushinda mabao 2-1, kwenye mchezo wa hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘CRDB BANK CUP’, uliochezwa juzi Jumatano (Aprili 03) Uwanja wa Nyankumbu, Geita.

Kitambi amesema katika mechi hiyo ilibidi waondoke uwanjani na mabao mengi, lakini baada ya kupata bao la pili tu, wachezaji wake wakaanza dharau.

Amesema atawaambia wachezaji wake siku nyingine wakiipata timu kama hiyo, inabidi wamalize mechi mapema.

Kocha Mkuu wa Rhino Rangers, yenye maskani yake Tabora aliwasifu wachezaji wake kwa kucheza kama alivyowaagiza, lakini tatizo lilikuwa ni viwango vya madaraja.

“Wachezaji walifanya kama nilivyoagiza, ila kwa bahati mbaya tumepoteza mchezo, sababu kubwa ni viwango, wenzetu kidogo wametuzidi daraja, lengo letu lililobaki sasa ni kucheza hatua ya nane bora ya Ligi Daraja la Pili kwa ajili ya kupanda Ligi ya Championship.

Rhino Rangers ni moja ya timu zilizofuzu hatua ya makundi ya ligi hiyo maarufu kama ‘first league’, ikishika nafasi ya pili kwenye Kundi B ikiwa na alama 27.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Aprili 6, 2024
Maamuzi ya Xavi yaipasua FC Barcelona