Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro ameliambia Bunge kwamba kwa sasa serikali imejikita katika ujenzi na ukarabati wa viwanja vitakavyotumika katika Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2027’.

Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Tarime Mjini, Michael Kembaki bungeni Dodoma aliyetaka kujua serikali ina mkakati gani wa kujenga uwanja wa michezo Wilaya ya Tarime.

“Kwa sasa serikali imejikita katika ujenzi na ukarabati wa viwanja vitakavyotumika katika Mashindano ya AFCON 2027” amesema.

Viwanja hivyo ni pamoja na ujenzi wa uwanja wa Arusha na Dodoma na ukarabati uwanja wa Benjamin Mkapa na Uhuru vilivyopo Dar es salaam.

Amesema serikali ipo tayari wakati wowote kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wamiliki na wadau mbalimbali wa michezo anaokusudia kujenga au kuboresha miundombinu ya michezo.

Kwa mujibu wa Ndumbaro, serikali itashirikiana na wadau mbalimbali kwa kuzingatia miongozo ya mashirikisho ya michezo husika ukiwemo uwanja wa Tarime, kama inavyoelekezwa na kifungu cha (7) na (iv) cha Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995.

Ten Hag, Garnacho waachiwa msala Man Utd
Polisi Arusha: Tumepokea maagizo ya Makonda