Serikali nchini, imesema haitafanya uzembe kwenye usimamizi wa ubora wa elimu na kuitaka Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), kuhakikisha inaendeleza udhibiti wa ubora wa elimu katika ngazi ya vyuo vikuu nchini.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ,Prof. Adolf Mkenda ameyasema hayo katika sherehe za siku ya Chuo Kikuu cha Iringa na kusema hakutakuwa na shinikizo lolote la utoajia wa Shahada zisizokidhi vigezo kwenye kazi za kitaaluma.
Amesema, lengo la kuanzishwa TCU ni pamoja na kuhakikisha inasimamia kwa weledi elimu ya vyuo vikuu nchini, kwa kufanya utambuzi na uidhinishaji wa elimu ya vyuo vikuu kabla ya chuo kikuu chochote kuanzishwa.
Waziri Mkenda amesema, ili kuwe na wataalamu wazuri katika sekta ya afya, ni vyema kuangalia uwezekano wa uwepo wa kuongezwa kwa vigezo hasa katika usimamizi wa masuala ya tiba unaoakisi ubora wa elimu.
“Tukicheza na ubora wa elimu tutaua nchi yetu, na hapa nchini vipo baadhi ya vyuo vya binafsi ambavyo ili viwe na wanafunzi wengi vinatoa GPA kubwa pasi na kujali ubora na uwezo wa wahitimu wao Tanzania sio kapu la kutuletea Digrii (Shahada) feki,”amesema.
Prof. Mkenda amebainisha kuwa, vigezo vya udahili na utoaji na ubora elimu vinafahamika, hivyo tathmini ikifanyika kwa uadilifu na vikaangaliwa vigezo kila mtu atapata halali yake kwa mujibu wa vigezo husika badala ya kuchkulia kawaida.
“Nchi yetu haiwezi kuendelea kwa kupeana nafasi kwa undungu, na kwa upendeleo ila tunaweza tukaendelea tukipeana nafasi kwa uwezo, vipaji na juhudi sio kwa sababu baba yako ana hela nyingi ndio upewe hiyo Hapana,” amesisitiza.
Waziri Mkenda amesema, mtu anaweza kuwa na akili nyingi lakini akawa mvivu na mlevi, licha ya kuwa na uwezo mkubwa lakini pia uzembe ukamtawala hivyo lazima TCU isimamie ubora na kufanya kazi kwa kasi ili Tanzania iwe na elimu bora.