Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amewataka Vijana katika kada mbalimbali nchini kutambua na kuthamini vipaji vyao ili waweze kufikia malengo waliojiwekea.
Katambi ameyasema Julai 23, 2022 wakati wa hafla ya uzinduzi wa Taasisi ya Mzalendo Project Foundation iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Jijini Dar es Salaam.
Amesema, azma ya Serikali ni kuendelea kuwajengea vijana mazingira wezeshi yatakayo wapatia fursa mbalimbali zitakazo wawezesha kujiajiri na kujikwamua kiuchumi.
“Serikali ipo tayari kutoa msaada utakaowapa vijana fursa za ajira na upatikanaji wa mitaji itakayo wawezesha kujishughulisha na kazi ambazo zitaweza kuwaingizia kipato,” alisema.
Katambi amesema, mikakati ya Serikali katika kusaidia vijana ikiwa ni pamoja na tafiti zilizofanyika kwa lengo la kuangalia namna nzuri ya kupunguza changamoto ya ajira.
Aidha, amefafanua hatua zilizochukuliwa na serikali kuhusu mabadiliko ya mitaala ili iendane na uzalishaji wa fursa za kuuwasaidia vijana kujiajiri, ikiwemo kupata maarifa ya kukabiliana na changamoto za ajira nchini.
Hata hivyo, Naibu Waziri Katambi amewapongeza vijana kwa namna wanavyojitoa na kujenga uthubutu wa kufanikisha malengo yao, hivyo amewataka vijana kutambua na kuthamini vipaji vyao ili waweze kutimiza ndoto na malengo kwa ustawi wa Taifa.
Awali, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mzalendo Project Foundation (MZPF), Enock Mwesiga alisema lengo lao ni kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana wa Vyuo vikuu nchini mara baada ya kumaliza elimu.
Amesema, “Pia tunawasaidia vijana kupata ufadhili wa kifedha kutoka taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi ili waweze kutimiza malengo ya mawazo yao ya kijasiriamali.”