Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wenye nia ya kutaka kuwekeza kwenye sekta ya utalii nchini, ili kuweza kutafsiri kwa vitendo maono ya Rais Samia kupitia filamu ya The Royal Tour
Waziri Chana ameyasema hayo, Jijini Dare s Salaam wakati akizungumza na Chama cha Mawakala wa usafiri wa anga Tanzania (TASOTA), kwenye mkutano wao wa mwaka ambapo kila mwaka unaowakutanisha mara moja kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali kuhusu ustawi wao.
Amesema, Serikali imepunguza ada ya kila mwaka kwa Mawakala wa Usafiri wa anga nchini (TALA fee), kutoka dola za Marekani 2,000 hadi dola 500 na kusema Serikali imejipanga kupunguza utitiri wa kodi katika sekta ya utalii, ili kuhamasisha Wawekezaji zaidi katika sekta hiyo na waweze kutoa ajira nyingi zaidi.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuwekeza miundombinu bora katika maeneo ya Hifadhi ikiwemo barabara zenye uwezo wa kupitika muda wote pamoja na usimikaji wa mtandao wa intaneti katika mlima Kilimanjaro.