Mwili wa Rais wa zamani wa Burkina Faso, Thomas Sankara na wasaidizi wake 12 waliouawa Oktoba 15, 1987 wakati wa jaribio la mapinduzi ya kijeshi, wamezikwa mahali walipouawa mjini Ouagadougou.
Katika Maziko hayo, mjane wa Thomas Sankara, Mariam Sankara na watoto wake wawili, ambao hawakukubali uchaguzi wa mahali pa kifo chake kwa maziko, hawakuwepo ingawa Viongozi wa serikali akiwemo Waziri Mkuu Apollinaire Joachimson Kyélem de Tambela, waliketi pamoja na wanafamilia.
Thomas Sankara, aliingia madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi mwezi Agosti 1983, na aliuawa Oktoba 15, 1987 wakati wa mapinduzi yaliyochochewa na naibu wake, Blaise Compaoré.
Siku ya tukio, Rais huyo wa Burkina Faso alikuwa katika mkutano kwenye makao makuu ya Baraza lake la Kitaifa la Mapinduzi (CNR), ndipo kundi la askari walipofika eneo hilo na kumpiga risasi yeye pamoja na wenzake 12.
Baadaye, miili ya Thomas Sankara na wasaidizi wake ilizikwa kwa mara ya kwanza kwenye makaburi yaliyopo nje kidogo ya mji wa Ouagadougou, Mei 25, 2015 kwa taratibu zote za kiitifaki.