Shirikisho la soka nchini Nigeria (NFF) limethibitisha timu ya taifa ya nchi hiyo Super Eagles itacheza michezo miwili ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Senegal na kisha Burkina Faso mjini London mwezi Machi.
Super Eagles wataanza kuwakabili Senegal (Teranga Lions) Machi 23 na siku nne baadae watacheza dhidi ya The Stallions (Burkina Faso).
Michezo hiyo ya kimataifa ya kirafiki imepangwa kuchezwa kwenye uwanja wa Hive uliopo Canons Park, ambao hutumiwa na klabu ya ligi daraja la nne Barnet FC.
Nigeria wanajipanga kucheza dhidi ya Senegal huku wakijivunia kuwa na rekodi nzuri dhidi ya taifa hilo la Afrika ya Magharibi, kwa kulishinda mara nane, kutoka sare mara tano na kupoteza mara tatu, katika michezo 16 iliyopita.
Kwa upande wa Burkina Faso, Nigeria haijawahi kupoteza katika michezo 13 iliyopita.
Nigeria wataitumia michezo hiyo ya kirafiki kwa ajili ya kujiandaa na harakati za kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia za mwaka 2018 pamoja na zile za Afrika za mwaka 2019.