Katika kuhakikisha kuwa mtandao wa wafanyabiashara na watumiaji wa dawa za kulevya unatokomezwa hapa nchini, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Jijini Mwanza, Marry Tesha amesema kuwa utekelezaji wa mapambano ya dawa hizo, uvuvi haramu vinatakiwa kupigwa vita na kila mtu ili kurejesha hali ya usalama na kuokoa nguvu kazi ya taifa ambayo imekuwa ikiangamia kila kukicha.
Ameyasema hayo jijini Mwanza wakati wa kikao cha uwasilishwaji wa taarifa kutoka kwa watendaji mbalimbali wa wilaya hiyo na kuongeza kuwa taarifa hizo bado hazijitosherezi hivyo kuwataka kuainisha mafanikio na mapungufu ya taarifa hizo.
Aidha, katika Kikao hicho kiliwahusisha viongozi mbalimbali ikiwemo polisi, uvuvi, Serikali za mitaa na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza ambapo taarifa ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana, OCD Ochieng Asiago, ilibainisha kukamatwa kwa watuhumiwa 15 na kesi 16 kutokana na dawa za kulevya.
Hata hivyo, kwa upande wake Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Mkoani Mwanza, Seth Mkemwa, amesema kuwa dawa zinazohisiwa ni za kulevya zinapokamatwa lazima zifikishwe ofisini kwa Mkemia Mkuu ili uchunguzi ufanyike na ikibainika ni dawa halisi watuhumiwa hufikishwa mahakamani mara moja.