WAZIRI wa Nchi- Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), George Simbachawene amezindua harambee ya uchangiaji wa Kampeni ya GGM Kili Challenge 2022 na kuahidi Serikali itaendelea kuthamini na kuwezesha jitihada za aina hiyo katika mapambano dhidi ya Ukimwi.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Weruweru wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, Simbachawene ameipongeza GGML ambao ni waanzilishi wa Programu ya ufadhili wa masuala ya VVU na UKIMWI kwa kupanda Mlima Kilimanjaro ambayo inatimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwake.
Amesema umuhimu wa afya bora kwa wananchi wa Tanzania ni moja ya vipaumbele vya Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kusema kwa jitihada hizo za GGML na wadau wengine kiwango cha upimaji wa VVU kimeongezeka kutoka asilimia 61 mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 81 mwaka 2020.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti – GGML anayesimamia miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo amesema mwaka huu wameendeleza mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, hivyo kwa kushirikiana na TACAIDS zoezi la kupanda mlima limeanza Julai 15 hadi Julai 21 mwaka huu.
“Tunawakaribisha sana wadau na makampuni mbalimbali kuchangia na kushiriki katika kampeni hii na tunaishukuru Serikali ya Tanzania kwa msaada wake na ushirikiano wa TACAIDS katika kampeni ya Kili Challenge tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002,” amesema Shayo.
Mkurugenzi Mkuu TACAIDS, Dkt. Leonard Maboko amesema licha ya mafanikio yaliyofikiwa, UKIMWI bado ni tatizo nchini na kwamba takwimu zinaonesha kuwapo kwa ongezeko la maambukizi mapya ya VVU hasa kwa makundi maalum yaliyo katika hatari kubwa ya maambukizi.
Hadi kufikia mwaka 2020 idadi ya Watanzania wanaoshi na virusi vya UKIMWI nchini imefikia watu 1,700,000 na Maambukizo mapya kwa mwaka ni watu 68,000.
“Makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya VVU ni vijana, wanaotumia madawa ya kulevya, wanaofanya biashara ya ngono, madereva wa malori yaendayo masafa marefu, wafanyakazi wa kwenye mashamba makubwa na jamii za wavuvi na wafanyakazi wa migodini. Makundi haya hatarishi yanahitaji mikakati maalumu ya kuzuia maambukizo mapya ya VVU kwao na kwa jamii kwa ujumla,” amefafanua Dkt. Maboko.
Naye, Meneja Mwandamizi wa masuala ya ubia kutoka GGML, Manace Ndoroma amesema shughuli za Kili Challenge ziliahirishwa kwa miaka miwili kutokana na ujio wa janga la UVIKO 19, mpaka pale ziliporuhusiwa tena na mamlaka husika mwezi April mwaka huu.
“Kwa sababu hiyo, maandalizi rasmi yalianza mwezi huo wa Aprili na ninayo furaha kukujulisha kwamba mbele yako kuna jumla ya washiriki 52, ikijumuisha wapanda mlima 24 na waendesha baiskeli 28. Ukilinganisha na jumla ya washiriki 55 kwa mwaka 2019, kuna upungufu wa watu 3 tu. Wote wametimiza vigezo vya ushiriki vinavyojumuisha vipimo vya afya na maandalizi ya kimwili (mazoezi),” amesema.
Kampeni ya GGM Kili Challenge ilianzishwa mwaka 2002 na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kwa lengo la kuchangia fedha kwa ajili ya shughuli za udhibiti wa ukimwi, ikiwa na lengo la kukusanya fedha ili kuisaidia serikali ya Tanzania katika jitihada zake kufikia malengo ya sifuri tatu.