Mamlaka za Ajira, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Wizara ya Afya pamoja na Sekretarieti ya Ajira Katika Utumishi wa Umma zimeagizwa kuhakikisha wanaendesha michakato ya ajira kwa uwazi, weledi, uadilifu pamoja na kutoa fursa sawa kwa waombaji wote kuweza kushiriki katika mchakato wa ajira hizi ili Serikali iweze kupata watumishi mahiri na wenye sifa stahiki.

Akizungumza hayo hii leo na waandishi wa habari Ofisini kwake Mtumba Jijini Dodoma Waziri wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama amesema utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya kuajiri watumishi wapya 44,096, kupandisha vyeo watumishi 92,619 na kubadilisha kada watumishi 6,026 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 umekamilika.

Amesema hatua ya kwanza ya mchakato wa kuhakikisha utekelezaji wa ajira hizo unakamilika kabla ya mwaka wa fedha 2021/22 haujaisha na Utekelezaji wa Ajira hizo utaigharimu Serikali kiasi cha shilingi bilioni 26.2 kwa mwezi sawa na Shilingi bilioni 570.4 kwa mwaka.

Mhagama ameongeza kuwa katika ajira hizo mpya Serikali imezingatia mgawanyo wa ajira katika Sekta mbalimbali zikiwemo Elimu, Afya, Kilimo, Maji, Mifugo, Uvuvi pamoja na maeneo mengine yenye uhitaji mkubwa wa watumishi ambapo Sekta ya Kipaumbele ya Elimu imetengewa jumla ya nafasi 12,035 ambapo Nafasi 9,800 kwa ajili ya Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari.

Huku Nafasi 2, 235 kwa ajili ya Wahadhiri wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Elimu ya Juu pamoja Wakufunzi wa Vyuo vilivyopo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Mchakato wa ajira hizi utasimamiwa na Taasisi husika za elimu kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma. 

Kwa upande wa Sekta ya Kipaumbele ya Afya imekasimiwa nafasi za ajira 10,285 zinazojumuisha nafasi 7,612 kwa ajili ya Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati zilizopo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Nafasi zingine 1650 kwa ajili ya kuajiri watumishi wa kada za Afya katika Hospitali za Kanda, Hospitali za Rufaa za Mikoa; Mchakato wa ajira hizi utasimamiwa na Wizara ya Afya huku Nafasi 1023 kwa ajili ya Vyuo vya Afya, Hospitali nyingine za kimkakati na zile za Mashirika ya Dini (District Designated Hospitals-DDHs) na Hiari ( Voluntary Agency-VAHs) zenye mkataba na Serikali ambapo Mchakato wa ajira hizo utasimamiwa na Wizara ya Afya kwa Vyuo vya Afya na Hospitali nyingine za kimkakati na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kwa Hospitali za DDHs na VAHs.

Nafasi 2,392 zinatarajiwa kujazwa kwenye Sekta zingine za kipaumbele ikiwa ni pamoja na Kada za Kilimo nafasi za ajira 814,Kada za Mifugo nafasi 700,Kada za Uvuvi nafasi 204,Kada za Maji nafasi 261 na Kada za Sheria nafasi 513 ambapo Mchakato wa ajira hizo utasimamiwa na Wizara pamoja na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.
Hata hivyo Nafasi zingine 7,792 kwa ajili ya kuajiri Watumishi wa kada nyingine kwenye Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi nyingine za Umma na Mchakato wa ajira hizi utasimamiwa na Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi nyingine za Umma pamoja na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

“Katika kutekeleza jukumu la Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Mishahara, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma ina dhamana ya kusimamia ajira za watumishi wa umma na mgawanyo na mtawanyo wake ndani ya Utumishi wa Umma, udhibiti wa Ikama na Bajeti ya mishahara, upandishaji vyeo pamoja na ubadilishaji wa kada kwa watumishi wa umma,” amesema Mhagama.

“Nichukue fursa hii kuwaasa waajiri na waombaji wa ajira mpya kujiepusha na vitendo vya rushwa na udanganyifu hususan wa vyeti vya elimu na taaluma wakati na baada ya mchakato wa ajira hizi.

Aidha Mhagama ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) kufuatilia kwa karibu mchakato mzima wa ajira hizi ili kuweza kubaini na hatimaye kuzuia mianya yote ya rushwa na upendeleo.

KMC FC kuwafuata Kagera Sugar, Geita Gold
Wanaokwamisha zoezi la Anuani za Makazi kuchukuliwa hatua