Wakati zoezi la uandikishaji wapiga kura likiendelea, Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT), imeonya vitendo vya rushwa, ubaguzi na unyanyapaa katika uchaguzi serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika nchini kote Novemba 24, 2019.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT), Elirehema Kaaya ametoa onyo hilo jijini Dodoma na kuongeza kuwa hawatarajii kuona vitendo vya rushwa na ubaguzi huku akiwataka wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kushiriki uchaguzi huo.
“Tunaonya watu kutojihusisha na vitendo vya rushwa ama ubaguzi wa aina yeyote uwe wa rangi ama kabila ama kijinsia na unyanyapaa wowote kwa mtu yeyote usiwepo katika uchaguzi huu wa mwezi novemba na hatutafumbia macho vitendo hivyo,” amefafanua Kaaya.
Kaaya amesema suala la unyanyapaa wa aina yeyote si suala la kiuungwana na kwamba uchaguzi huo ni muhimu kwani unampa mtu haki ya kidemokrasia kumchagua Kiongozi anayemtaka na ambaye atasimamia shughuli za maendeleo za eneo husika ikiwemo suala la ulinzi na usalama.
“Tangu tarehe 8 ya mwezi Oktoba zoezi hili limeanza na litaendelea hadi tarehe 14 ya mwezi huu wa Oktoba hivyo wananchi wasisite kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na hata wale watakaogombea wanatakiwa pia kufanya hivyo ili wawe na sifa stahiki na ni vyema fursa hiyo ikatumika ipasavyo na tukapata viongozi watakaotufaa kimaendeleo,” ameongeza Katibu Mkuu huyo.
Hata hivyo Kaaya amefafanua kuwa kadi ya mpiga kura haitatumia kupigia kura katika uchaguzi huo wa Serikali za mitaa isipokuwa sifa pekee ni kuhakikisha wale wote watakaoshiriki zoezi hilo wanajiandikisha katika vituo mbalimbali vilivyo karibu na makazi yao.
“Maeneo yote ambayo kuna matangazo ya kuhamasisha kujiandikisha hata yale ya magari yanayotangazia wananchi yawe yanatoa taarifa sahihi na kama ni maandishi basi yawe yameandikwa kwa maandishi yanayosomeka vizuri ili kuepusha taarifa zenye upotoshaji,” amesema.
Zoezi la uandikishaji wa wapiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, lilianza rasmi Octoba 8, 2019 na linatarajia kumalizika Oktoba 14, 2019 huku uchaguzi huo ukitarajiwa kufanyika Novemba 24, 2019 nchini kote.