Klabu ya Azam FC imeitumia salama Young Africans, kwa kuitaka ijiandae kuitema nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, endapo watashindwa kufikia lengo la kutwaa ubingwa msimu huu 2020/21.

Young Africans imejizatiti kwenye nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, baada ya kuichabanga Ruvu Shooting mabao matatu kwa mawili jana Alhamis, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Azam FC, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ amejivisha ujasiri wa kutuma salamu hizo, kwa kuamini kikosi chao kina kila sababu ya kuishusha Young Africans katika nafasi ya pili.

Azam FC hadi sasa ipo nafasi ya tatu huku ikiwa na alama 60 katika msimamo wa ligi ikiongozwa na Young Africans yenye alama 64 huku kinara akiwa ni Simba mwenye 67.

Zaka Zakazi amesema kuwa upo uwezekano mkubwa kwao kupata nafasi ya pili endapo watashindwa kufikia lengo la kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu.

“Maandalizi ya kumalizia mechi zetu zilizobaki bado yanaendelea kama kawaida na lengo letu ni kuhakikisha tunachukua nafasi ya pili kama tutakosa kuchukua ubingwa wa msimu huu.”

“Kwa upande wa kikosi kipo salama kambini isipokuwa baadhi ya wachezaji ambao waliumia katika mchezo wa kirafiki Never Tigere na Bryson Raphael lakini pia na Prince Dube ambaye ana malaria,” amesema Zaka Zakazi.

Mtambo wao wa mabao ndani ya Ligi Kuu ni Prince Dube ambaye ametupia mabao 14 na pasi tano za mabao akiwa ni namba moja kwa utupiaji Bongo.

Sabaya afikishwa Mahakamani wananchi wamzomea
Wachina wakimbia Mahakamani baada ya kufutiwa kesi na DPP