KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrka Mashariki na Kati, Azam FC, kimewasili salama jijini Dar es Salaam saa 10.45 Alfajiri ya leo kikitokea nchini Zambia kilipotwaa ubingwa wa michuano maalumu ya kimataifa ya timu nne iliyofanyika katika Uwanja wa Levy Mwanawasa jijini Ndola.

Azam FC imetwaa ubingwa huo mbele ya timu tatu nyingine, wenyeji Zesco United ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu Zambia waliomaliza katika nafasi ya tatu kwa pointi nne, Zanaco FC walioshika ya pili kwa pointi tano, huku mabingwa wa Zimbabwe, Chicken Inn wakikamata mkia kwa pointi moja.

Matajiri hao wa viunga vya Azam Complex, walianza kwa kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Zesco kabla ya kuinyuka Chicken Inn mabao 3-1 na kumaliza michuano hiyo kwa kutoa suluhu walipochuana na washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Zambia, Zanaco.

Mara baada ya Azam FC kutua leo ilipokewa na mashabiki kadhaa wa timu hiyo waliokesha ndani ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere kuwasubiri, ambao waliwapongeza wachezaji kwa mafanikio hayo waliyopata.

Kutokana na umuhimu wa mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Mwadui ya Shinyanga utakaofanyika Jumatatu ijayo, kikosi cha Azam FC kimefikia moja kwa moja kambini ndani ya viunga vya Azam Complex.

Kwa mujibu wa programu ya benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu Stewart Hall, kikosi cha Azam FC leo kitapumzika kabla ya kesho saa 2.30 kuanza mazoezi ya kujiandaa ya mchezo huo.

Benchi hilo kwa kiasi kikubwa limeridhishwa na michuano hiyo waliyotoka kushiriki na limeweka wazi ya kuwa itawasaidia kufanya vizuri kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo inapewa nafasi kubwa  ya kukutana na Bidvest Wits ya Afrika Kusini mwezi ujao.

Azam FC mpaka sasa kimejikusanyia jumla ya pointi 39 katika nafasi ya tatu sawa na Simba walio nafasi ya pili, zote zikidiwa pointi moja na kinara Yanga mwenye pointi 40, lakini Wanajangwani na Wekundu hao wako mbele michezo miwili zaidi ya Azam FC.

Hivyo kama Azam FC ikifanikiwa kushinda mechi zake mbili za viporo dhidi ya Tanzania Prisons Februari 24 na Stand United Machi 16 mwaka huu, itaweza kuwashusha chini wapinzani wake hao kwenye mbio za ubingwa na kukaa kileleni.

TFF Yaonya Upangaji Wa Matokeo
Serikali yaweka sawa, CT-Scan ya Muhimbili ilihamishwa kutoka UDOM