Wanamuziki wa Kongo, Nguza Vicking ‘Babu Seya’ na mwanae Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ ambao wako gerezani, wamezungumzia taarifa zilizoenea mtandaoni kuwa waliandika barua kuomba msamaha kwa Rais John Magufuli.

Wakizungumza katika mahojiano maalum na gazeti la Risasi ndani ya gereza, mahojiano yaliyosimamiwa na Mkuu wa Gereza la Ukonga, ACP Stephen Mwaisabila, wanamuziki hao walikanusha kumuandikia barua Rais Magufuli.

“Ukweli ni kwamba, barua niliandika mimi mwaka 2010. Ilikwenda kwa Rais Kikwete (Jakaya, wakati huo). Lakini tangu pale sijawahi kuandika tena barua. Hiyo inayosambaa mtandaoni ni ileile inajirudia. Kwa Magufuli hatujawahi kuandika barua,” Papii aliliambia gazeti hilo.

Naye Mkuu wa Magereza hiyo, ACP Stephen Mwaisabila alionesha kushangazwa na habari zinazoandikwa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu hali ya wafungwa hao maarufu na kuvitaka kuacha kutunga habari.

Katika hatua nyingine, Babu Seya alikanusha habari zilizoenezwa kuwa yuko hoi na hupelekwa katika Hosptali ya Taifa ya Muhimbili mara kwa mara. Alisema kuwa huwa anaumwa ugonjwa wa kisukari na sio kweli kwamba huyo hoi.

“Ninapoonekana Muhimbili (hospitali), huwa nakwenda kliniki. Kwa hiyo siyo kweli kwamba nakuwa hoi. Kisukari ni ugonjwa kama magonjwa mengine na nimeupata kama wanavyoweza kuupata watu wengine ambao hawapo gerezani,” anakaririwa.

Wawili hao ambao wameendelea kusisitiza kuwa wanaamini siku moja watatoka gerezani, mwaka 2004 walihukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kuwalawiti watoto.

Wamekata rufaa katika Mahakama ya Haki za Binadamu Afrika yenye makao yake Arusha wakipinga maamuzi ya Mahakama ya Rufaa.

Nicki Minaj amvaa Kanye West kwa alichokiimba kuhusu wanawake
Ajali yasababisha kifo cha Mkurugenzi Wizara ya Afya