Kamati ya Maadili ya Shirikisho la soka nchini Tanzania ‘TFF’ kesho Jumamosi (Mei 21) itakutana jijini Dar es salaam kusikiliza mashauriu mawili, yaliyowasilishwa mbele yake na klabu za Simba SC na Young Africans.

Kwa mujibu wa taarifa iliyothibitishwa na TFF kupitia kurasa zake za Mitandao ya Kijamii, kamati hiyo itakutana kujadili malalamiko yaliyowasilishwa na pande zote mbili, huku kila upande ukidai kuchafuliwa na mwenzake.

Upande wa Young Africans unadai kuchafuliwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC Barabara Gonzalez kupitia Kituo cha Radio cha Afrika Kusini, kwa kutoa shutuma zisizo za kweli dhidi ya klabu hiyo, hivyo kuchafua taswira yao mbele ya umma.

Nayo Simba SC imemlalamikia Afisa wa Young Africans Haji Manara, kwa madai kuwa kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, alitoa shutuma zisizo za kweli dhidi ya klabu yao, hivyo kukiuka kanuni za maadili za TFF, Toleo la 2013.

Tayari Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ameielekeza Sekretarieti ya TFF kuhakikisha walalamikiwa wote wamepewa mashtaka dhidi yao, pamoja na mwito wa kuhudhuria mashauri hayo, ambayo yalianza kusikilizwa tangu Mei 14, 2022.

Kwa mantiki hiyo, Kikao cha kesho Jumamosi (Mei 21) ni mwendelezo wa kamati ya maadili ya TFF kusikiliza mashauri hayo.

Ukarabati mkubwa wafanywa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid
Jeshi la Polisi lazungumzia raia aliyejeruhiwa kwa risasi