Mkutano Mkuu Maalum wa CCM uliopangwa kufanyika wikendi hii umeonekana kuwa neema ya kipekee kwa wakazi wa mji wa Dodoma hususan wafanyabiashara za vyakula na hoteli kutokana na matumizi makubwa yatakayofanywa na chama hicho.

Ikiwa ni takribani mwaka mmoja wa ukimya wa biashara za hoteli mjini humo huku baadhi zikidaiwa kufungwa, CCM imetangaza kukodi hoteli 306 kwa ajili ya watu 3,331 watakaohudhuria mkutano huo wenye lengo la kulipigia kura jina la Rais John Magufuli kuwa Mwenyekiti mpya wa chama hicho.

Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka jana aliwaambia waandishi wa habari kuwa hotel zote 306 na maeneo mengine yataimarishiwa ulinzi na kwamba mji huo kwa ujumla utakuwa salama.

“Dodoma ni shwari na salama watu wasiwe na hofu na tuna imani mkutano utamalizika vizuri,” alisema Ole Sendeka.

Aidha, Msemaji huyo wa CCM alisema kuwa jumla ya wajumbe 2,456 wanatarajiwa kupiga kura ya kumchagua Mwenyekiiti wa chama hicho na kwamba watakuwa na nafasi ya kupiga kura ya ‘Ndio au Hapana’.

“Tuna imani wajumbe wote watampa mwenyekiti mpya kura zote za ‘ndio’ ili achukue nafasi ya kuongoza kitaifa,” alisema.

Katika hatua nyingine, Ole Sendeka alisema kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana pamoja na Manaibu Katibu Wakuu wawili na watendaji wengine watajiuzulu nafasi zao ili kumpa nafasi Mwenyekiti Mpya (Rais Magufuli) kupanga safu yake.

“Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana atakabidhi barua yake kwa mwenyekiti wa chama kupisha Rais Magufuli aweze kuunda safu yake ya watu atakaofanya nao kazi,” Ole Sendeka anakaririwa.

Alisema kuwa chama hicho ni madhubuti na kwamba chama madhubuti huunda Serikali madhubuti lakini chama legelege huunda serikali legelege.

BAVICHA wavimba tena, ‘hatuogopi’
Vigogo 12 wa NSSF watumbuliwa Jipu