Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inadaiwa kuuza shule ya Sekondari ya Tegeta inayoimiliki na kulazimika kuwahamisha wanafunzi wa kidato cha tano na sita waliokuwa wakiendelea na masomo shuleni hapo. Imedaiwa kuwa mauzo hayo yamefanywa bila kufuata taratibu(Kinyemela).

Tuhuma hizo zilizochapishwa na Mwananchi zimeeleza kuwa chanzo cha kuaminika kimesema kuwa shule hiyo imeuzwa kwa Chuo Kikuu cha Mzumbe na kwamba malipo yamefanyika kwa awamu mbili.

Akizungumzia tuhuma hizo, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Abdallah Bulembo amesema kuwa hawajaiuza shule hiyo bali Chuo Kikuu cha Mzumbe kimefidia gharama za majengo yaliyopo. Hata hivyo, alikiri kuwa umiliki wa shule hiyo umehamia kwa Chuo Kikuu cha Mzumbe na umebarikiwa na Baraza la Wadhamini la Jumuiya hiyo.

Akieleza sababu ya kuchukua hatua hiyo, Bulembo alisema kuwa shule hiyo ni kati ya shule zake ambazo hazifanyi vizuri na zinaweza kufa mbeleni huku akitaja sera ya Elimu Bure kama mojawapo ya changamoto iliyoikabili katika kuendesha shule hiyo binafsi.

“Tuna shule nyingi zaidi ya 60, baadhi zimekumbwa na matatizo ikiwamo kutofanya vizuri, hivyo tuna mkakati wa kuziondoa ili huko mbele zisije zikafa kabisa. Serikali imetangaza elimu bure uanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne. Hivi nikuulize wewe [Mwandishi], mwanao akifaulu utaacha kumpeleka huko? Lazima tuangalie mbele ndiyo maana tumefikia uamuzi huu,” Bulembo anakaririwa na Mwananchi.

Kufutia uamuzi huo, baadhi ya wanafunzi wameeleza kufikwa na sintofahamu ya hatma ya masomo yao kwani wakiulizwa huelezwa kuwa shule haijauzwa, majibu ambayo wanadai ni tofauti na uhalisia.

Wanafunzi hao walifika katika Ofisi ndogo za CCM, zilizoko Lumumba jijini Dar es Salaam kufikisha kilio chao. Mwanafunzi mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema kuwa baada ya kufanya kikao na uongozi ofisini hapo, walielezwa kuwa shule haijauzwa bali imebadilishwa matumizi kuwa chuo.

Bulembo aliwaondoa hofu wanafunzi wa kidato cha sita kuwa kwakuwa wanasubiri kufanya mtihani wao wa kuhitimu mapema mwakani, wamepanga kuwahamishia katika shule nyingine.

“Hawa wa kidato cha sita wao tunawatafutia shule nyingine ambayo watafanya mitihani yao ya mwisho kwa kutumia namba ya Tegeta [Sekondari],” alisema Bulembo.

Frank Lampard Kurejea Stamford Bridge
The Gunners Wajizatiti Kwa Mesut Ozil