Kiongozi wa chama cha ACT WAZALENDO, Zitto Kabwe amewataka wananchi wa mkoa wa Kagera kuchagua viongozi watakaosaidia kuukomboa mkoa huo kiuchumi na watakaoweza kusimamia vyema na kukamilisha miradi iliyokwama kwa mda mrefu, ikiwemo ujenzi wa kituo cha mabasi (Stendi), Bukoba.
Zito ameyasema hayo katika mkutano wa siasa wa chama hicho Mkoani Kagera, kilichofanyika Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba katika ziara yake ya kutembelea mikoa 16 ya Tanzania bara.
Amesema, “kuna mikoa mingine sasa hivi hawazungumzii stendi za mkoa, wanazungumzia stendi za wilaya nyie bado mnaangaika na stendi lakini endeleeni kuvumilia tu muhimu ni kujipanga tuhakikishe miradi yote iliyokwamishwa na hao watu ambao hawajali mambo ya maendeleo inafufuliwa na ili iweze kuendelea.”
Aidha, ameongeza kuwa, “hakuna sababu ya mkoa wa Kagera kuwa mwisho kwa kipato kwasababu umepakana na nchi mbalimbali kuna haja ya kuufanya kuwa kituo cha biashara hali itakayosaidia kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na mkoa kwa ujumla.”