Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile amewashukia wanasiasa wanaotaka kuwagawa Watanzania wanapojadili suala la makubaliano ya Ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu uendeshaji wa bandari kadhaa nchini ikiwemo ya Dar es Salaam.
Mbunge huyo ameyasema hayo kufuatia mjadala unaoendelea kuhusu ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai ambapo baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakiujadili kwa misingi wa u-Tanzania Bara na Uzanzibar.
Amesema, “natoa rai kwa wanasiasa wote nchini wanaojadili suala hili la bandari kuepuka kutumia maneno yenye kuibua hisia za ubaguzi, chuki na kuhatarisha amani na mshikamano wetu kama Taifa chini ya Rais Samia Suluhu Hassan tumeshuhudia uzalendo wake, nia yake njema kwa Taifa hili na namna anapambana kwa maslahi ya nchi yetu.”
Aidha, ameongeza kuwa “wote ni mashahidi kazi kubwa na nzuri inafanyika awamu hii ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika uwazi wa mikataba na mashirikiano mbalimbali, tunaingia kama Taifa na yote inapitia bungeni kuonyesha nia njema ya Rais Samia Suluhu Hassan.”
“Tupuuze propaganda chafu, siasa za uongo, ubaguzi na fitina. Tusimame pamoja na Rais Samia katika kusimamia maslahi mapana ya nchi yetu. Natoa Rai kwa Watanzania kuwapuuza wanasiasa wanaohubiri siasa za kibaguzi na chuki,” amesema Ditopile.