Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amewataka wataalam wa afya na elimu na wengine wote kutumia elimu yao kuwaelimisha wengine juu ya elimu ya usonji.

Amesema hayo wakati akifungua hafla ya uelimishaji jamii kuhusu Usonji, iliyoambatana na uchangishaji fedha kwa ajili ya kuwawezesha vijana wenye usonji kupata mafunzo ya kilimo mahiri yaliyoandaliwa na Lukiza Autism Foundation, Jijini Dar es Salaam.

“Nitoe rai kwa wataalam wetu wa afya na elimu au wawakilishi wao, madaktari, Ustawi wa jamii, walimu wa watoto wenye uhitaji maalum, waandishi wa habari na wengine wote mlioshiriki katika hafla hii, kutumia elimu na uelewa uliopatikana leo kuwaelimisha wengine” Amesema Dkt. Gwajima.

“Tanzania, takwimu zilizopo ni za idadi ya Watoto wenye usonji waliofanyiwa usaili katika shule maalum na wale walioonwa katika vituo vya kutolea huduma. Takwimu za mwaka 2018 zinaonesha kuwa, wanafunzi 1416 wana Usonji na walimu 157 katika shule 18 za Msingi”, ameeleza Waziri Gwajima.

Dkt. Gwajima ametoa wito kwa Taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Kiserikali kufanya tafiti kuhusu tatizo la usonji, na kuweka wazi kuwa, Serikali itatoa ushirikiano kuhakikisha kuwa tafiti hizi zinafanyika na matokeo ya tafiti hizo yanatumika kuimarisha huduma kwa watoto wenye Usonji nchini.

“Ninatoa wito na kuhimiza Taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Kiserikali kufanya tafiti kuhusu tatizo la usonji na serikali itatoa ushirikiano kuhakikisha kuwa tafiti hizi zinafanyika na matokeo ya tafiti hizo yanatumika kuimarisha huduma kwa watoto wenye Usonji”, ameeleza Waziri Gwajima. 

Nembo rasmi miaka 60 ya Uhuru Tanzania
Madanguro Tanga marufuku.