Migogoro ndani ya vyama vya ushirika nchini, imetakiwa kutatuliwa kwa haraka kwa lengo la kuondoa uzoroteshaji wa majukumu ya vyama na kuleta uzalishaji wenye tija.
Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ali wakati akifungua mafunzo ya usimamizi wa vyama vya ushirika katika Kanda ya Mashariki kwa maofisa 78 wa ushirika wa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.
Amesema, Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania – TCDC, inatakiwa kuhakikisha inafanya kazi kwa karibu na Mamlaka za Serikali, ili kuhakikisha inaboresha maisha ya wananchi kupitia ushirika.
Aidha ameongeza kuwa, vyama vya ushirika vinatakiwa kujikita katika kuongeza thamani ya mazao na bidhaa zinazozalishwa ili kujipatia fedha zaidi zikiwemo za kigeni kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi na wa vyama vya ushirika.