Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amekutana na kufanya mazungumzo na Menejimenti ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania – TACAIDS, yaliyolenga kuufahamu muundo na utendaji wa Tume, ikiwa ni sehemu ya ratiba yake kukutana na Idara na Taasisi zote zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Akizungumza na Waandishi wa habari hii leo Machi 10, 2023 Jijini Dodoma, Dkt. Yonazi ameipongeza Tume kwa kazi nzuri wanazofanya na kueleza ni muhimu kuongeza kasi zaidi katika kuyafikia malengo na kuhakikisha jamii inapata huduma na elimu kadiri iwezekanavyo.
Amesema, “Ninawapongeza TACAIDS kuendelea kusaidia katika mapambano haya na kila jitihada zinazofaywa zina tija katika kuyafikia malengo hivyo, tuendelee kutoa elimu kwa umma kwa kuzingatia kuwa mnayagusa maisha watu.”
Aidha, ameongezea kuwa Ofisi yake ipo wazi na itaendelea kutoa ushirikiano kwa Tume hiyo kwa kuzingatia umuhimu wa shughuli zinazotekeleza na Tume.