Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imefungua rasmi Ofisi za Ubalozi wa Tanzania Jijini Windhoek, nchini Namibia.

Akihutubia katika hafla ya ufunguzi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax ameishukuru Wizara ya Mambo ya Nje kwa ushirikiano ya Namibia ilioutoa katika hatua zote za kuanzisha ofisi hizo, pamoja na kushiriki tukio la kihistoria la ufunguzi ambalo ni hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax.

“Wakati huu ambapo Serikali za Tanzania na Namibia zipo kwenye mazungumzo ya lugha ya Kiswahili kuwa sehemu ya lugha ya chaguo katika shule za Namibia, Ubalozi umefungua maktaba ndogo yenye vitabu na majarida ya Kiswahili kwa ajili ya watu wenye nia ya kujifunza kiswahili kuja kujisomea,” amesema Dkt. Tax.

Kwa upande wake, Netumbo katika hotuba yake alisema kwa sasa nchi hizo mbili zina makazi ya ubalozi katika miji mikuu ikiwa na lengo la kukuza na kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo pamoja na watu wake na kumpongeza Balozi wa Tanzania nchini Namibia, Dkt. Modestus Kipilimba kwa kuchagua jengo lenye ubora na la kisasa kwa ajili ya ofisi za ubalozi huo.

Jiji la Windhoek nchini Namibia.

Amesema, “Tanzania ikiwa mpambanaji wa Bara la Afrika na Kusini mwa Afrika siku zote imekuwa pamoja nasi na hivyo sisi wanamibia tutakapokuja kujisomea na kufanya tafiti katika maktaba hii ya Kiswahili inayofunguliwa leo tutakuwa katika mazingira salama.”

Hafla ya ufunguzi wa ofisi hizo, imefanywa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax na kulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Tanzania na Namibia wakiwemo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah, Mabalozi wa nchi za Afrika na viongozi wa jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini humo.

Vipers SC yamfungashia virago Bianchi
Sidibe wa Real Bamako amtaja Fiston Mayele