Unyeshaji wa mvua chini ya wastani tofauti na matarajio, umesababisha hofu ya kutopata chakula cha kutosha kwa Wananchi wa baadhi ya maeneo mkoani Dodoma, baada ya mazao yaliyopandwa kushindwa kuvunwa kulingana na matarajio.
Hayo yamesemwa wakati wa kikao cha wadau wa kilimo wa Halmashauri zote nane za Mkoa kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule hii leo Machi 31, 2023 kujadili namna ya kukabiliana na tishio la njaa, endapo suluhisho la haraka halitafanyika.
Akielezea mwenendo wa Hali ya hewa kwa Mkoa wa Dodoma kwa msimu huu, Mtaalamu kutoka Mamlaka ya Hali ya hewa nchini, Isdor Kirenga amesema Dodoma ilitabiriwa kupata mvua chini ya wastani na ilitarajiwa kuanza wiki ya pili ya mwezi Januari hadi Aprili 25 ambapo pia TMA ilitabiri uwepo wa vipindi vya ukame.
Kufuatilia hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amewataka wataalamu kutoa matarajio ya tathmini ya chakula kwa Mkoa na kusema, “tujitathmini matarajio yetu ya chakula yakoje kutokana na maelezo ya wataalamu, hali ni mbaya kwenye Halmashauri zetu. Wataalamu mtuambie makadirio ya mahitaji ya chakula kwa Mkoa.”
Aidha, amewagiza Wakuu wa Wilaya kusimamia kila Halmashauri na kuweka mkakati wa namna ya kukabiliana na tishio la upungufu wa chakula na kuchukua tahadhari kabla ya shari. Senyamule ametoa rai kwa wakazi wa Dodoma kujifunza namna ya kuweka akiba ya chakula na kutafuta suluhisho la kudumu kama Mkoa.
Awali, Afisa Kilimo Mkoa wa Dodoma, Abraham Benard, amesema Mkoa ulijiwekea malengo ya kulima hekta 7 za chakula lakini mvua hazikunyesha kama ilivyotarajiwa kwani zimenyesha mvua chache kwa siku nyingi na mvua nyingi kwa siku chache hivyo kuathiri upatikanaji wa chakula kama ilivyotarajiwa hali iliyopelekea Serikali kutoa mahindi ya bei nafuu jumla ya tani 12,747.15
Hata hivyo, Idara ya Kilimo imetoa mapendekezo kadhaa ya kukabiliana na hali hii ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya kina ya mazao yaliyopo kwa sasa kupata kiasi kilichovunwa na kuweka akiba ya kutosha. Wananchi wanahimizwa pia kufuga mifugo midogo midogo kama kuku kwani wanaweza kusaidia kupambana na upungufu wa chakula.