Ukosefu wa elimu ya ndoa, umetajwa kuwa ni moja kati ya changamoto inayopelekea kuwa na ongezeko la matukio ya ukatili na unyanyasaji kwa wanandoa na Watoto katika familia.
Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa Dawati la Jinsia na Watoto Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, ACP Faidha Suleiman wakati akizungumza na Wachungaji wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mwanga Mkoani Kilimajaro, waliotembelea Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Jijini Dodoma kwa lengo kujitambulisha na kujifunza mambo mbalimbali ya kiusalama.
Amesema, baadhi ya watu huingia kwenye taasisi ya ndoa bila kuielewa vyema taasisi hiyo kwa kukosa elimu ya kutosha hali ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa uwepo wa matukio ya ukatili kwa wanandoa wenyewe na watoto kwakuwa pindi maelewano yanapokosekana ndani ya ndoa huweza kusababisha wanandoa hao kufanyiana vitendo vya ukatili.
Aidha, ACP Faidha ametoa wito kwa Wachungaji hao kwenda kuanzisha madawati ya jinsia na watoto katika himaya zao, ili kutoa nafasi kwa waumini wao kueleza changamoto zao na kupatiwa msaada kwa wakati kabla ya kuleta madhara makubwa.
Kwa upande wao Wachungaji hao pamoja na kushukuru Jeshi la Polisi kwa elimu waliyoipata pia wameomba kupatiwa semina za mara kwa mara, ili kuwa na uelewa wa pamoja katika kuzuia matukio ya ukatili wa kijinsia na watoto.