Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF), umesema umeridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa
Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia (EBARR) unaotekelezwa katika
Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma, na kusimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Hayo yamesemwa hii leo Jumatano (Februari 15, 2022) na ujumbe wa Mfuko huo ukiongozwa na
Mratibu wa GEF Kanda ya Afrika, Dkt. Ibrahima Sow wakati wa ziara ya kutembelea Mradi huo
katika Vijiji vinne vya Wilaya hiyo.
Amesema, GEF imedhirisha na utekelezaji wa miradi hiyo ambayo ni ujenzi wa visima
virefu vinne, malambo mawili, majosho mawili, vitalu nyumba vitatu na mashine ya kukamulia
alizeti ambapo miradi hiyo imeweza kuwa chanzo mbadala cha kuongeza kipato kwa wananchi.
“Miradi hii ina faida kubwa kwa wananchi wa Mpwapwa, natoa rai kwa jamii kuweza kuitunza
na kuwasaidia kwa ajili ya kuleta manufaa ya sasa na kwa kizazi kijacho” amesema Dkt. Sow
ambaye aliambatana na ujumbe kutoka Sekretarieti ya GEF.
Sow ameongeza kuwa, GEF itaendelea kufadhili miradi ya mazingira inayozunguka jamii ili kuongeza
kasi ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira katika maeneo ya vijijini sambamba kuhakikisha
jamii inajishughulisha na kilimo rafiki kwa mazingira na kutolea mfano kilimo cha mbogamboga.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa EBBAR Kitaifa, Dkt. Makuru Nyalobi amewataka
wananchi wa Wilaya hiyo kusimamia vyema miradi hiyo ya maendeleo inayotekelezwa katika
maeneo yao ambayo inatarajia kuwanufaika wananchi wa vijiji vya Nghambi, Mbugani, Kiegea
na Kazania.