Wafanyakazi wanawake wa Kampuni ya Geita Gold Mine Limited (GGML), wameendesha semina ya siku mbili kwa ajili ya kutoa malezi ya kitaaluma kwa wanafunzi wa kike mkoani Geita, ikiwa ni jitihada za kuhakikisha jamii inanufaika kutokana na shughuli za uchimbaji dhahabu nchini.

Akizungumza kwa niaba ya menejimenti ya GGML, Meneja Mwandamizi wa Mawasiliano na Mahusiano, Manace Ndoroma amesema wanawake wanaofanya kazi mgodini, wamekuwa mstari wa mbele kuhamasisha umuhimu wa nafasi ya mwanamke katika jamii.

Amesema, GGML kupitia umoja huo imekuwa ikitoa misaada mbalimbali ikiwemo fedha na vifaa mbalimbali kwa makundi maalumu ndani ya jamii yetu ili kuhakikisha jamii inayozungukwa na shughuli za uchimbaji wa dhahabu inafaidika kutokana na uwepo kampuni hiyo.

 Baadhi ya wanafunzi wa Sekondari ya bweni ya wasichana ya Nyankumbu wakiwasikiliza viongozi na wafanyakazi wanawake wa Kampuni ya GGML ambao waliwapatia mafunzo ya siku mbili kuhusiana na malezi ya kitaaluma kwa wanafunzi hao wa kike mkoani Geita. 

“Tumekuwa mstari wa mbele kushirikiana na Serikali kuhamasisha masuala ya usawa wa kijinsia. Mtakumbuka tarehe 26 Agosti mwaka huu ilikuwa siku ya usawa wa wanawake duniani. GGML tulitoa elimu kubwa kwenye mitandao yetu ya kijamii na vyombo vya habari juu ya nafasi muhimu ya mwanamke katika jamii.

Amesema, “Tumekuwa tukifanya hivyo pia hata katika matukio ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kila tarehe 8 Machi,” alisema Ndoroma na kuongeza kuwa semina hiyo ni mwarobaini wa changamoto za wanafunzi wa kike kufahamu taaluma sahihi za kuchagua katika maisha baada ya kuhitimu elimu ya sekondari.”

Awali, akitoa hotuba katika eneo hilo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Prof. Godius Kahyarara amewataka wadau mbalimbali nchini kuchangia maendeleo ya elimu nchini hususani kwa mtoto wa kike badala ya kuiachia serikali jukumu hilo pekee yake.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita, Zahara Michuzi (kushoto) akizungumza katika mafunzo ya kuwapatia malezi ya kitaaluma wanafunzi wa kike mkoani Geita. Katikati ni Mkuu wa Shule ya Sekondari ya bweni ya wasichana ya Nyankumbu, Georgia Mugashe  na kulia ni Meneja Mwandamizi – Mawasiliano na Mahusiano kutoka GGML, Manace Ndoroma.

Amesema, “Nawapongeza sana GGM kwa kuonyesha mfano mzuri wa wadau wanaochangia maendeleo ya elimu. Bahati nzuri nchi yetu imeendelea kuwa na mfumo mzuri wa elimu bora ukilinganisha na nchi zingine. GGM wanao mchango mkubwa katika uchumi wa nchi yetu kutokana na kodi wanayolipa.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita, Zahara Michuzi ameipongeza GGML na wafanyakazi wanawake wanaofanya kazi katika kampuni hiyo kwa kuandaa mafunzo hayo yanayotoa mwangaza kwa wanafunzi wengi wa kike kujitambua na kufikia malengo sawa na viongozi wa kike waliofanikiwa katika nafasi mbalimbali.

GGML, imekuwa kinara wa uwekezaji kwenye jamii tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000 ambapo vipaumbele vikuu vimekuwa ni miradi ya afya, elimu, maji, barabara, miradi ya kukuza kipato na miradi mingine mingi ya kijamii ili kuhakikisha jamii mwenyeji inapata maisha bora.

Picha ya pamoja baada ya semina hiyo.

Kampuni hiyo imejenga zaidi ya shule saba za Msingi na tano za Sekondari ndani ya Mkoa wa Geita kwa kipindi cha miaka minne iliyopita na Semina hiyo, ilifanyika katika Shule ya Sekondari yabweni ya wasichana ya Nyankumbu iliyojengwa na GGML, ikiasisiwa na kampuni hiyo kupitia Umoja wa Watumishi Wanawake wanaofanya kazi mgodini, GGM ladies.

Pasuwa: Ni vigumu kuifunga Simba SC Dar es salaam
Nyumba yateketea, 35 wanusurika kifo