Kocha Mkuu wa Klabu Bingwa nchini Malawi ya Nyasa Big Bullets Callisto Pasuwa ni kama amekata tamaa kuelekea mchezo wa Mkondo wa Pili wa Hatua ya Awali (Ligi ya Mabigwa Barani Afrika) dhidi ya Simba SC ya Tanzania.

Big Bullets ilipoteza mchezo wa Mkondo wa Kwanza nyumbani juzi Jumamosi (Septemba 10) kwa kufungwa 2-0, na kujiweka katika mazingira magumu kuelekea mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, mwishoni mwa juma hili.

Pasuwa amesema mchezo wa Mkondo wa Pili utakua mgumu, kutokana na mazingira ya mchezo huo, ambapo wenyeji wao Simba SC wana kasumba ya kutokubali kufungwa wanapocheza Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Amesema katika mchezo wa Jumamosi waliipa Simba SC heshima kubwa katika kipindi cha kwanza, na ndipo walipofanya makosa makubwa ya kujikuta wakipoteza dhidi ya timu hiyo ya Dar es salaam.

“Tuliipa Simba SC heshima kubwa katika kipindi cha kwanza ambayo ni moja ya sababu zilizotufanya kupoteza mechi tukiwa nyumbani. Haitakuwa rahisi kwetu Tanzania.”

“Ni ngumu sana kushinda Dar es salaam kwa sababu tunajua Simba SC wanapokua katika Uwanja wa Mkapa wana Rekodi nzuri sana, ni kama tumeshapoteza mchezo kabla ya kuanza safari, lakini hatuna budi kwenda kucheza na kuonyesha upinzani dhidi yao.” amesema Pasuwa

Nyasa Big Bullet italazimika kusaka ushindi wa mabao matatu kwa sifuri ama zaidi, ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, kinyume na hapo itakuwa imetolewa kwenye Michuano hiyo Mikubwa katika ukanda wa Bara la Afrika upande wa Vilabu.

Azam FC yawasili salama jijini Mbeya
GGM Ladies yawapa malezi ya kitaaluma Wanafunzi wa kike