Katika kuimarisha mahusiano baina ya Serikali na jamii, Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) na Taasisi ya Rafiki Surgical Mission ya Australia wametoa msaada wa magari mawili ya kubeba wagonjwa kwa Halmashauri ya wilaya ya Geita mkoani Geita.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano huko Nzera mkoani Geita, Mkurugenzi Mkuu wa GGML, Terry Strong amesema GGML kwa kushirikiana na Shirika la Rafiki Surgical mission wameamua kutoa magari hayo ili kuokoa maisha ya wagonjwa katika halmashauri ya Wilaya hiyo.
Amesema, “Halmashauri ya Wilaya ya Geita iliomba magari mawili ya kubebea wagonjwa kutoka GGML kwa ajili ya kusaidia jamii ya eneo hilo kwa sababu baadhi ya wagonjwa walikuwa wakipata rufaa ya kwenda Hospitali ya Rufaa ya Geita ambayo iko mbali na Nzera na maeneo mengine ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita.”
Aidha Terry ameongeza kuwa, “GGML na Rafiki Surgical Mission walijibu ni washirika wazuri wa maendeleo, wanasaidia miradi ya afya katika kipindi cha miaka 20 iliyopita na kwa pamoja tumekuwa na ushirikiano tangu mwaka 2000 kupitia upasuaji wa mdomo sungura na zaidi ya wagonjwa 1700 wamenufaika na mpango huo.”
Ameongeza kuwa, GGML ilitumia zaidi ya Shilingi bilioni 5 katika miundombinu ya afya na usambazaji wa vifaa tiba kwa kipindi cha miaka 20 ya uendeshaji na kusaidia ujenzi wa hospitali, ukamilishaji wa vituo vya afya zaidi ya 10, vituo vipya vya afya vinne, uboreshaji wa kituo cha afya cha Kasota, usambazaji wa vifaa tiba vya vituo vya Katoro na Bukoli vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya na mkoa wa Geita.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo amesema msaada wa GGML umekuja wakati muafaka kwani utaokoa maisha ya wagonjwa huku akiwataka wadau wa Halmashauri hiyo kushirikiana na Serikali kukabiliana na changamoto za kiafya kwamba tangu kuanzishwa kwa GGML imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Serikali, hususan Halmashauri za Wilaya na Miji ya Geita kusaidia miradi mbalimbali endelevu ya jamii.