Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya klabu ya Simba, Zacharia Hans Poppe amesema kikosi cha klabu hiyo kitaendelea kuwa pamoja hadi watakaporejea katika Ligi Kuu Bara.

Mwenyekiti huyo amesema kuwa wameamua kufanya hivyo ili kuhakikisha kikosi chao kinaendelea kuwa pamoja na fiti. Aliongeza kuwa Kikosi cha timu hiyo kitaendelea na maandalizi mfululizo, ikiwezekana kucheza zaidi mechi za kirafiki.

Kikosi cha Simba kinatarajia kurejea jijini Dar es salaam hii leo, kikitokea jijini Arusha kilipokwenda kucheza mchezo wa robo fainali ya kombe la shirikisho dhidi ya Madini FC, na kuibuka na ushindi wa bao moja kwa sifuri.

Jana jioni Simba walicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Mererani Stars katika Uwanja wa CCM Mererani, Arusha.

Katika mchezo huo Simba waliibuka na ushindi wa bao moja kwa sifuri, lililofungwa na mshambuliaji kutoka nchini Ivory Coast Frederick Blagnon mapema kipindi cha kwanza akimalizia pasi ya mshambuliaji mwenzake, Hajja Ugando.

Wachezaji wa Simba watakua na mapumziko ya siku mbili, kabla ya kurejea katika mazoezi ya kujiandaa na michezo ya ligi kuu ambayo watacheza kanda ya ziwa wakianza na Kagera Sugar mjini Bukoba, kisha wataelekea jijini Mwanza kucheza na Mbao FC na watamaliza na Toto Africans kwenye uwanja wa CCM Kirumba.

Mgeja ang'aka kuhusu tuhuma za Bulembo
Gwajima Ajitetea Mahakamani, adai polisi alitaka kumchoma sindano