Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman amesema Tanzania haiwezi kuepuka mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kijamii na ya Teknlolojia, kwa kuwa ndio yanayoakisi siasa za Ulimwengu.
Othman ameyasema hayo mjini Zanzibar, wakati akifunga mkutano wa Wadau wa Demokrasia uliojadili masuala ya Zanzibar yanayohusu vyama vingi vya Siasa.
Amesema, kwamba siasa za Dunia ya sasa ni ushindani, ubunifu na ufanisi na iwapo nchi itashindwa katika masuala hayo inaweza kuwa ni msindikizaji na hivyo ni vyema kuicha historia ya kisiasa nchini kuwa mwalimu, lakini sio izuie nchi kusonga mbele.
Aidha, Othman amewaeleza washiriki hao kwamba kuna umuhimu kama taifa kujiuliza sababu za mageuzi yanayohitajika ndani ya nchi na kukubalika na wananchi na kwamba mtazamo wa kimageuzi lazima ufanane kifikra kwa wananchi wote ili kuweza kufikia mageuzi ya kweli ya kidemokrasia.
Aidha, amefahamisha kwamba maegeuzi ni muhimu katika kufanyika katika ustawi wa kiuchumi hasa kwa vile Zanzibar ikitegemea suala la biashara ya huduma na bidhaa, lakini kwa kutegemea uwekezaji wa fedha nyingi sambamba na utaalamu ili kuvutia uwekezaji utakaoleta mabadiliko ya kweli ya kiuchumi.
Mkutano huo, wa Wadau wa Demokrasia kujadili masuala makhusuri yanayohusu vyama vingi vya Siasa umeitishwa kufuatia agizo la Rais Mwinyi, kutaka kujadiliwa masuala hayo kutokana na umuhimu wake kwa Zanzibar.