Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Cameroon Hugo Broos amesema anafanya kazi pasina mkataba, tangu mwezi Februari mwaka huu, ikiwa ni siku kadhaa baada ya kuiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa Afrika nchini Gabon.

Kauli hiyo ya kufanya kazi bila mkataba, imetolewa na kocha huyo kutoka nchini Ubelgiji, alipozungumza na waandishi wa habari katika mkutano maalum, ambao ulilenga kutangaza kikosi chake, kitakachocheza mchezo wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia dhidi ya Algeria ugenini.

Broos amesema mpaka sasa hajafahamu hatma yake kuhusu suala la kusaini mkataba mpya na viongozi wa shirikisho la soka nchini Cameroon, na badala yake anaendelea kufanya kazi kama kawaida.

“Sifahamu lolote linaloendelea,” alijibu Broos baada ya kuulizwa na waandishi wa habari.

Hata hivyo kocha huyo amesema suala la mkataba litaendelea kuwa njia panda kwa upande wake, lakini dhamira kubwa aliyojiwekea ni kuiwezesha Cameroon kufuzu fainali za kombe la dunia za 2018.

“Tunahitaji kushinda, siamini kama hili linaweza kunikwamisha katika dhamira niliyojiwekea, lengo langu ni kumaliza kwenye nafasi ya kwanza katika kundi.

“Kuna suala la viwango vya ubora wa soka, pia ninalizingatia sana katika utendaji wangu wa kazi, nitajivunia kama nitaiwezesha Cameroon kushika nafasi za juu kwenye viwango vya ubora wa soka duniani ambavyo hutolewa na FIFA kila mwezi.”

Broos atalazimika kushinda mchezo dhidi ya Algeria bila ya kuwa na mshambuliaji wa klabu ya Stoke City Eric-Maxim Choupo-Motin pamoja na Karl Toko Ekambi wa klabu ya Angers ya Ufaransa, ambao wote kwa pamoja wamejiondoa kikosini.

Choupo-Moting amemuarifu Broos kuhusu jeraha linalomkabili katika kipindi hiki, ili hali Ekmabi amesema wazi haitaji kuitumikia timu ya taifa ya Cameroon kwa sasa.

“Siwezi kufafanua kwa kina kwa nini wachezaji wanagoma kurejea nyumbani kwa ajili ya kuitumikia timu yao ya taifa, endapo sababu ni kutokupenda kuichezea timu hii, basi hawajakomaa katika weledi. Alisema Broos

Kikosi cha Cameroon kilichotangazwa na Broos tayari kwa mchezo dhidi ya Algeria upande wa makipa: Fabrice Ondoa (Sevilla, Spain), Jules Goda (Ajaccio, France) na Georges Bokwe (Mjondalen, Norway)

Mabeki: Michael Ngadeu Ngadjui (Slavia Prague, Czech Republic), Adolphe Adolphe (FC Sochaux, France), Ernest Mabouka (Maccabi Haifa, Israel), Jean-Charles Castelleto (Brest, France), Serge Leuko (CD Lugo, Spain), Collins Fai (Standard Liege, Belgium), Yaya Banana (Panionios, Greece) na Tolo Nouhou (Seattle Sounders, USA)

Viungo: Georges Mandjeck (Sparta Prague, Czech Republic), Sebastien Siani Siani (KV Oostende, Belgium), Franck Zambo Anguissa (Marseille, France) na Olivier Boumal (Liaoning Whowin, China)

Washambuliaji: Clinton Njie (Marseille, France), Vincent Aboubakar (FC Porto, Portugal), Benjamin Moukandjo (Jiansung, China), Christian Bassogog (Henan Jianye, China), Jean Pierre Nsame (Young Boys, Switzerland), Ngameleu Moumi (Rheinorf, Austria), Fabrice Olinga (Royal Mouscron, Belgium) na Frantz Pangop (Union de Douala, Cameroun)

Mchezaji jeuri arejeshwa kikosini Burkina Faso
Lema, Nassari wawasilisha ushahidi Takukuru