Msanii wa Vichekesho, Idris Sultani na mwenzake wameachiwa huru baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuleta shahidi zaidi ya mara mbili.

Uamuzi huo wa kuwaachia huru umetolewa leo Mei 17, 2021 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashid Chaungu.

Sultan anakabiliwa na tuhuma ya kushindwa kusajili laini ya simu inayomilikiwa na mtu mwingine na mwenzake Innocent Maiga anayeshtakiwa kwa kushindwa kutoa taarifa.

Wakili wa Serikali Silvia Mitanto alidai kesi hiyo leo ilikuja kwa ajili ya kusikilizwa lakini hawana shahidi sababu siku ya tarehe ya kesi Mei 14 ilikuwa sikukuu ya Eid.

Wakili wa utetezi, Jebra Kambole amepinga hoja hiyo kwa madai kwamba haina msingi, shauri la muda mrefu hivyo aliomba wateja wake waachiwe huru.

Baada ya kusikiliza hoja hizo Hakimu Chaungu alisema sababu ya upande wa Jamhuri haina msingi na kwamba Februari 22 mwaka huu alitoa ahirisho la mwisho, tangu hapo hakuna shahidi hadi Aprili 29 mwaka huu ambapo pia hawakuwa na shahidi.

“Kwa mazingira hayo mahakama inalifuta shauri hili chini ya kifungu cha sheria namba 225 , washtakiwa wanaachiwa huru,” amesema na kuwaachia huru washtakiwa.

Rais: Haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyimwa
Kamati ya Corona yapendekeza chanjo itumike kwa hiari