Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo ametoa siku 30 kwa Mameneja wa Kanda zote, Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira -NEMC, kuendesha kampeni za kuondosha mifuko ya plastiki isiyoruhusiwa kisheria, inayochangia ongezeko la uchafuzi wa mazingira hasa maeneo ya mijini.
Akitoa tamko la Serikali kuhusu katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki katika mkutano wake na waandishi wa habari leo Aprili 6, 2023 Dkt. Jafo amesisitiza kuwa Meneja yoyote wa NEMC atayeshindwa kudhibiti matumizi ya mifuko hiyo katika eneo lake atatakiwa kuachia ngazi mara moja na kuwaachia watendaji wenye uwezo wa kutimiza wajibu huo.
Amesema, katika siku za hivi karibuni kumejitokeza changamoto ya matumizi ya vifungashio vya plastiki kutumika kubebea bidhaa na matumizi ya mifuko isiyoruhusiwa kisheria, kinyume cha Kanuni ya 6 ya Kanuni za Kupiga Marufuku Mifuko ya Plastiki za Mwaka 2019 na hivyo kuibua changamoto ya usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya miji.
“Vifungashio hivyo, vinakosa sifa na hivyo kutokidhi matakwa yaliyowekwa na Shirika la Viwango Tanzania -TBS. Hali hii inachangia katika ongezeko la uchafuzi wa mazingira hususan maeneo ya mijini na hali hii inaonesha ukiukwaji mkubwa wa Kanuni ya kupiga marufuku mifuko ya plastiki unaofanywa na baadhi ya wazalishaji na wasambazaji,” amesema Waziri Jafo.
Aidha, ameiasa jamii na kueleza kuwa ni makosa kisheria kubadili matumizi ya vifungashio hivyo kuwa mifuko ya kubebea bidhaa, na kwa mujibu wa sheria, adhabu stahiki zitatolewa kwa wanaokiuka sheria wakiwemo watengenezaji, waingizaji, wasambazaji na watumiaji wa vifungashio vya plastiki vilivyozalishwa ama kuingizwa nchini na kutumika kama vibebeo vya bidhaa.
Jafo pia amezitaka Sekretarieti za Mikoa, Majiji, Manispaa na Halmashauri za Wilaya zote nchini kuendelea kudhibiti matumizi ya vifungashio visivyoruhusiwa kisheria kwa kuzingatia kuwa utekelezaji wa katazo la mifuko ya plastiki ni jukumu la wadau wote.
Juni Mosi, 2019 Serikali ilipiga Marufuku uzalishaji, uingizaji nchini, usafirishaji nje ya nchi; usambazaji na matumizi ya mifuko ya plastiki kutumika kama vibebeo na vifungio katika bidhaa mbalimbali.