Jaji wa Mahakama ya juu ya Marekani Amy Coney Barrett, ameapishwa baada ya kupigiwa kura na baraza la Seneti lililogawanyika pakubwa, ambapo Warepublican waliwazidi nguvu Wademocrat na kumuidhinisha Barret.

Chaguo la Trump kujaza nafasi iliyoachwa kufuatia kifo cha aliyekuwa jaji wa kiliberali marehemu Ruth Bader Ginsburg, kimsingi linafungua enzi mpya ya maamuzi kuhusu utoaji mimba, ulinzi wa huduma za afya na hata kuchaguliwa kwa Trump mwenyewe.

Wademocrat walishindwa kuzuia matokeo hayo, ambayo ni jaji wa tatu kuchaguliwa na Trump kwenye mahakama hiyo, wakati Warepublican wakiendelea na harakati za kuifanyia mageuzi idara ya mahakama.

Barret mwenye umri wa miaka 48 ameanza kazi rasmi, ikiwa ni uteuzi wake wa maisha wa kuwa jaji wa 115 na kuimarisha nguvu za mahakama ya juu kuegemea mkondo wa mrengo wa kulia.

Akizungumza wakati wa hafla ya kumuapisha Barrett ameapa kufanya kazi yake bila hofu wala upendeleo.

“Ahsante pia kwa Seneti kwa kutoa idhini yake kwa uteuzi wangu, ninashukuru kwa imani mliyonionesha na ninaahidi kwenu na kwa watu wa Marekani kuwa nitatekeleza majukumu yangu kwa uwezo wangu wote” amesema Barrett.

Kura hiyo ya Seneti ni ya kwanza kufanywa karibu mno na uchaguzi wa rais, na ya kwanza katika nyakati za sasa kufanywa bila uungwaji mkono kutoka kwa chama cha wajumbe wachache ambapo Barrett alipigiwa kura 52 dhidi ya 48.

Barrett, jaji wa Mahakama ya Rufaa kutoka jimbo la Indiana, anatarajiwa kula kiapo cha mahakama leo kitakachoongozwa na Jaji Mkuu John Roberts katika sherehe ya faragha ili kuanza kushiriki katika shughuli za mahakama hiyo.

Azam FC wakubali shughuli ya Mtibwa Sugar
Nampesya: Anayofanyiwa Morrison sio sahihi