Serikali imetangaza kuwa kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi ni siku maalum ya usafi nchi nzima kama ilivyokuwa katika siku ya Desemba 9 mwaka huu kufuatia agizo la rais John Magufuli.

Akitoa tamko hilo la serikali mbele ya waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam,

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina alisema kuwa uamuzi huo umefikiwa ili kuhakikisha kunakuwa na utamaduni wa kudumu wa kufanya usafi wa mazingira ili kuepuka magonjwa ya milipuko.

“Lengo kuu ni kuepusha mitaa yetu kupata magonjwa ya milipuko kama kipindupindu na kujitengenezea utamaduni wa uwajibikaji binafsi wa kutunza mazingira yetu,” alisema Mpina.

Aliongeza kuwa wizara yake imeweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kufanya ufatiliaji kwenye maeneo yote nchini.

Alisema kuwa kutokana na hali isiyoridhisha ya usafi, watu waliougua kipindupindu mwaka 2015 ni takribani watu 12,000 huku watu 194 wakiripotiwa kufariki kutokana na kipindupindu.

“Zoezi hili ni la lazima kwa kila mtanzania bila kujali nafasi zao au ushawishi wao kwenye jamii, wote wanawajibika,” alisema.

Afande Sele: Kufanya Video Afrika Kusini ni Ulimbukeni
Askari Polisi Amuua Askari Mwenzake Kwa Risasi na Kisha Kujilipua