Waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali vya Kenya na Kimataifa, wameshambuliwa na genge la watu wenye silaha eneo la Kibra nchini humo, wakati wakiripoti maandamano ya kwanza ya kila wiki ya kupinga serikali kwa kushindwa kushughulikia upandaji wa gharama za maisha.
Kwa mujibu wa kituo cha Habari cha Citizen Digital, kimeeleza kuwa katika tukio hilo Waandishi wengine kadhaa walijeruhiwa na genge hilo lilokuwa likirusha mawe katika eneo la DO Kibra.
Citizen imeripoti kuwa, Mwandishi wa Habari Jase Ndung’u alipohojiwa alisema, “tulipokuwa tukiangazia maandamano yaliyokuwa yakiendelea, waandamanaji walikuwa wamewasha mioto mikali na tulikuwa tukitazama maandamano yakiendelea tuliposhambuliwa na Genge hilo lilijifanya kuwa sehemu ya waandamanaji lakini walikuwa na silaha.”
Aidha, baadhi ya waandishi ambao hawakuweza kukimbia waliibiwa vitu vyao huku wengine wakiachwa na majeraha na hata hivyo Jeshi la Polisi lilirusha vitoa machozi kutawanya maandamano hayo ya Jumatatu yaliyoitishwa na upinzani ukiapa kuendeleza maandamano licha ya marufuku ya Polisi.
Hata hivyo, Kinara mkongwe wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga amewataka watu kujitokeza barabarani kila Jumatatu na Alhamisi, hata baada ya maandamano wiki moja iliyopita kuwa na vurugu na kupooza kwa baadhi ya maeneo ya Nairobi.