Beki wa kulia wa Young Africans Kibwana Shomari amesema hana taarifa zozote kuhusu kusajiliwa kwa beki na nahodha wa AS Vita Djuma Shaban, kama inavyoelezwa katika vyanzo mbalimbali vya habari nchini Tanzania.

Kibwana ambaye ni chaguo la kwanza kwenye kikosi cha Young Africans tangu aliposajiliwa akitokea Mtibwa Sugar mwanzoni mwa msimu huu, amesema uhakika wa kusajiliwa kwa beki huyo anaecheza nafasi yake hajaupata, na hana papara ya kuupata katika kipindi hiki ambacho ameelekeza akili yake katika kuisaidia klabu ya Wananchi.

Amesema hata kama itathibitisha Djuma atajiunga na Young Africans kwa msimu ujao, hana shaka na hilo kwa sababu lengo ni kuisaidia klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, kufanya vizuri katika ligi ya Tanzania na kimataifa.

“Sina taarifa za usajili wa mchezaji huyo, lakini hata kama atakuja sio mbaya kwani akija wote lengo letu litakuwa ni kutimiza malengo ya Young Africans.”

“Najikubali na nipo hapa kuitumikia timu hii (Young Africans), hivyo nitashirikiana na kila mchezaji aliyepo na atakaekuja kwa lengo la kufanikisha malengo ya timu, kuhusu ushindani wa namba nadhani siwezi kuzungumzia maana hayo ni maamuzi ya kocha ndiye ataamua ampange nani,” amesema Kibwana.

Taarifa zinaeleza kuwa jana Alhamisi Uongozi wa Young Africans ulikamilisha mpango wa kumsjili Djuma Shaban huko mjini Kinshasa, DR Congo, na wakati wowote atawasili nchini kukamilisha taratibu nyingine za uhamisho wake.

Rwanda Air yasitisha safari zake Uganda
Zahera: Nipo tayari kuisaidia Young Africans