Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Mtibwa Sugar Thobias  Kifaru amesema hakuna wa kulaumiwa, baada ya kikosi chao kukubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Simba SC.

Jana Alhamis (Juni 23) Mtibwa Sugar ilikua ugenini katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, katika mchezo wa Mzunguuko wa 28 wa Ligi Kuu Tanzania.

Kifaru amesema kilichotokea katika mchezo huo ni sehemu ya matokeo ya soka, na ilikua ngumu kwao kuweza kuifunga Simba SC iliyo kwenye kiwango bora katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa msimu huu 2021/22.

Amesema Simba SC imekua na kiwango kizuri zaidi tangu alipoondoka Kocha Franco Pablo Martin, imeshinda michezo yake miwili kabla ya kukutana na Mtibwa Sugar jana Alhamis (Juni 23).

“Tumecheza vizuri sana, lakini haikuwa rahisi kuifunga Simba SC iliyo katika kiwango bora kama hiki, wamecheza michezo miwili kwa uwezo mkubwa kabla ya kukutana nasi, tulijua tunakuja kucheza na timu ya aina gani,”

“Hakuna wa kumlaumu kwa hili lililotukuta hapa Dar es salaam, kilichotokea ni sehemu ya mchezo, tunarudi nyumbani kujiandaana mchezo wa Namungo FC ambao tunaamini tutaendelea kupambana na kupata matokeo mazuri.” Amesema Kifaru

Kwa ushindi huo Simba SC imefikisha alama 60 zinazoendelea kuiweka nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu, ikitanguliwa na Young Africans yenye alama 70 kileleni.

Mtibwa Sugar yenye alama 31, imeendelea kushika nafasi ya 12 ikisaliwa na michezo miwili dhidi ya Namungo FC Uwanja wa Manungu Complex mkoani Morogoro, kisha itamaliza msimu kwa kucheza na Young Africans Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Simba SC itamaliza michezo yake ugenini dhidi ya Tanzania Prisons katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na kisha watapambana na Mbeya Kwanza FC kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma.

Kifaru: Nilitabiri ubingwa Young Africans, Simba imekosea
Simba SC yawashukuru Mashabiki kwa Mkapa