Aliyekua Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya klabu ya Simba, Hamis Kilomoni ameibuka na kuuponda mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo chini ya muwekezaji Mohamed Dewji *Mo*.

Kilomoni na kundi lake ambalo lilikua likipinga mchakato wa mabadiliko na baadae kumpinga muwekezaji Mohamed Dewji, amesema kwa mandhari ndani ya klabu ya Simba mambo si shwari kutokana na uongozi wa klabu hiyo uliochaguliwa na wanachama kuwekwa pembeni.

Kilomoni amesema wanachama ambao wana asilimi 51 ya hisa za klabu ya Simba SC walifanya uchaguzi na kuchagua viongozi wao kikatiba, lakini hadi sasa hakuna anaewasemea, zaidi ya upande wa “Mo” ambao umekua mstari wa mbele katika kusema na kuendesha mambo ya klabu hiyo.

“Klabu yetu ya Simba ama klabu ya Young Africans ni klabu za watu, tena watu sio wadogo, klabu hizo zimegawanyisha Tanzania pande mbili, sio kama klabu nyingine zenye watu wachache, hivyo tunatakiwa kuziheshimu.”

“Kwa sasa mimi na kundi langu tumeamua kunyamaza, lakini ukweli ni kwamba uendeshaji wa klabu yangu hauendi vizuri, kwa sababu wanachama wa klabu wamefanya uchaguzi wa viongozi kwa asilimia 51, lakini upande wa asilimi 49 ya muwekezaji ndio inaongoza na kufanya shughuli za kila siku za klabu yetu, sasa kwa hali hii inaonyesha dhahir mambo hayapo sawa.”

“Leo viongozi waliochaguliwa kwa nguvu ya wanachama hawana lolote wanalolifanya, zaidi ya kushiriki kwenye vikao vya bodi, lakini utendaji wote umeachwa upande wa muwekezaji mwenye asilimia 49, jambo ambalo sio sahihi, tulipaswa kuona waliochaguliwa kwa nguvu ya wanasimba wanashiriki katika shughuli za kiutendaji.”

Katika hatua nyingine Hamis Kilomoni amewatumia ujumbe baadhi ya wadau wa soka wanaonyooshea vidole kwa kumtazama kama mtu mwenye uchu wa fedha na madaraka ndani ya klabu ya Simba, ama mpinga maendeleo ndani ya klabu hiyo ambayo kwa sasa imeonyesha kuwaneemesha mashabiki kwa kupata matokeo mazuri ndani ya uwanja.

“Hakuna ninachokitafuta Simba SC, kwa sababu mimi nimeshamaliza hatua zote ndani ya Simba SC, nimekua mchezaji, kiongozi na mdhamini wa klabu, sasa nihitaji nini ndani ya hii klabu?” Alihoji Kilomoni.

“Ninachotaka kuona mimi ni klabu inaendeshwa kwa misingi ya usawa, nataka kuona wanachama wenye klabu yao wanashirikishwa kupitia uongozi waliouchagua, sio kumuachia mtu mmoja afanye anavyotaka.”

Azam FC: Simba SC waje mezani
Serikali yaingilia kati hatma Maghorofa yaliojaa maji Mbweni