Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Zambia chini ya umri wa miaka 20 Conlyde Luchanga ametangaza njaa ya kusaka kiatu cha dhahabu katika fainali za kombe la dunia kwa vijana, ambazo zitaanza mwishoni mwa juma hili Korea kusini.

Luchanga ametangaza matamanio ya kutaka kuwa mfungaji bora katika fainali hizo ambazo zitashirikisha mataifa mbali mbali duniani.

Akihojiwa na shirika la utangazaji la nchini kwao Zambia akiwa kambini huko Hispania, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 19 amesema, atapambana kila awezavyo ili kufanikisha ndoto alizojiwekea katika fainali za kombe la dunia kwa vijana.

Amesema anafahamu mtihani huo aliodhamiria kuushinda sio rahisi kutokana na umahiri wa wachezjai wengine watakaokutana nao, lakini ukweli ni kwamba, anaamini kila hatua atakayoipiga itakua na mafanikio makubwa kutokana na ushirikiano mzuri uliojengeka kikosini mwao.

Katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya kikosi cha vijana cha klabu ya Las Palmas uliochezwa jumatatu na Zambia kuibuka na ushindi wa mabao manne kwa sifuri, Luchanga alifunga goli moja na kufikisha mabao matatu tangu walipoanza kambi ya kujiandaa na fainali za kombe la dunia.

Kocha mkuu wa kikosi cha Zambia chini ya umri wa miaka 20, Chambeshi amekiri kufurahishwa na mwenendo wa mshambuliaji huyo na amemuunga mkono katika ndoto zake za kutaka kuwa mfungaji bora wa michuano ya dunia.

Katika hatua nyingine mshambuliaji huyo wa klabu ya Lusaka Dynamos, amesifia mazingira ya kambi ya kikosi cha Zambia kwa kusema ni mazuri na anaamini yanawajenga kisaikologia, ili watakapofika kwenye fainali za kombe la dunia huko Korea kusini wafanikishe azma ya kufanya vyema.

Katika fainali za kombe la dunia chini ya umri wa miaka 20 Zambia imepangwa katika kundi la C sambamba na mataifa ya Ureno, Iran na Costa Rica.

JPM afanya uteuzi mwingine leo Mei 17, 2017
Polokwane City Kumng'oa Donald Ngoma Jangwani