Kocha wa Simba, Jackson Mayanja sasa ameingia kwenye ugomvi mkubwa na Mganda mwenzake, mshambuliaji Hamisi Kiiza.

Mayanja amemfukuza Kiiza kambini Ndege Beach, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam kwa shutuma za utovu wa nidhamu.

Mayanja anamshutumu Kiiza kukataa kupanda basi la timu na kuvaa sare kwenda uwanja wa taifa, Dar es Salaam kushuhudia mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga na Al Ahly.

Wachezaji wote wa Simba walikuwepo jukwaani siku ya jumamosi katika uwanja wa taifa na sare zao, fulana na suruali nyekundu za kimichezo wakati Yanga ikitoa sare ya 1-1 na wapinzani wao wa kihistoria.

Alipotafutwa Kiiza kuzungumzia sakata hilo, akasema anaona kama anatafutiwa sababu ya kuchafuliwa jina.

“Mimi naona kama wanataka kunigombanisha na timu. Jana asubuhi tumemaliza mazoezi (Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini), tukaambiwa jioni tutaingia kambini, lakini kwanza tutakula chakula cha mchana pamoja na kwenda Uwanja wa Taifa,”.

Kiiza anasema kwamba Meneja wa timu, Abbas akaagiza wachezaji wote wavae sare wakati wa kukutana kwa chakula cha mchana na wasije na gari zao, kwa sababu watapanda basi la timu.

Hata hivyo, Kiiza anasema kwamba alimfuata kocha Mayanja na kumuambia kwamba ameitwa kwenye kikao na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Kassim Dewji hivyo anahisi atachelewa chakula cha mchana cha pamoja.

“Mayanja akaniambia hayo mimi hayanihusu, mwambie Meneja. Mimi nikamuambia Meneja, akanielewa nikaondoka zangu,”anasema Kiiza.

Anasema alikwenda kukutana na Dewji katika kikao kilichodumu hadi Saa 9:15 Alasiri ndipo wakaachana na kwa sababu muda ulikuwa umekwenda sana, akaamua kwenda Uwanja wa Taifa moja kwa moja ili akitoka ndiyo arejee nyumbani kwake kuchukua sare na vifaa vya kambini.

“Baada ya mechi Abbas akanipigia kuniambia Kiiza usije kambini kwa sababu umekataa kupanda basi la timu na kuvaa sare. Mimi nikashangaa sana, kwanza muda mwingi tunapokuja mazoezini tukitokea nyumbani huwa hatubebi sare. Na hata Juuko (Murshid) na (Jonas) Mkude hawakuja na basi la timu pia,”

“Lakini mimi nikamuambia Abbas kama unataka nisiingie kambini, mwambie bosi (Dewji) aniambie hivyo kwa sababu yeye ndiye shahidi yangu nilikuwa naye kwenye kikao. Abbas akasema sitaki kujua hayo. Mimi nikampigia Dewji kumuambia, yeye (Dewji) akawapigia akina Abbas. Akanirudia mimi akaniambia niende kambini na yeye anakuja. “Nilipofika kambini, Mayanja akanikuta akaniuliza, Abbas amekupa ujumbe wako? Nikamuambia amenipa, lakini Dewji amezungumza naye nadhani ameelewa, ikawa kama yamekwisha,” amesema Kiiza.

Baadhi ya wachezaji wa Simba wakiwa na sare zao Uwanja wa Taifa jana

Amesema kwamba baadaye wakafanya kikao cha timu na kuruhusiwa kwenda kulala, naye akaenda chumbani kwake. “Baadaye (Nahodha Mussa Hassan) Mgosi akanifuata chumbani kuniambia Abbas kasema niondoke kambini, nikamuambia siondoki, wakashindwa, waliposhindwa wakamleta mchezaji wa timu B aje alale kwenye chumba changu, tukalala naye,”.

“Asubuhi wakasema baada ya chai kuna kikao. Kwenye kikao wakaanza kuongea kwa mafumbo, mimi nikawaelewa na baada ya kikao wakasema Kiiza ondoka kambini haumo kwenye programu mechi ya kombe la TFF dhidi ya Coastal Union.”

“Nikamuambia Abbas, unanionea mimi kwa nini? Mkude na Juuko mbona hawakuja na basi la timu? Mmeanza ugomvi na mimi, mnataka kunichafulia jina, nikaondoka kwenye kikao nikaweka vitu vyangu kwenye gari.”

Kiiza anasema baada ya hapo, akampigia simu Dewji kumtaarifu juu ya kufukuzwa kwake tena kambini kwa sababu zile zile. “Dewji akashangaa, akanifokea kabisa anasema; ‘rudi kambini, hilo suala nimekwishaongea nao tangu jana na likaisha’. Ndiyo sasa nimerudi kambini nasubiri mengine,”amesema Kiiza.

Kocha Mayanja na Meneja Abbas wote hawakupatiana kwenye simu zao walipotafutwa, wakati Dewji simu yake ilikuwa inaita bila majibu.

Kiiza anakuwa mchezaji wa tatu ndani ya mwezi mmoja na ushei kugombana na Mayanja, baada ya awali kutofautiana na beki Hassan Isihaka na kiungo Abdi Banda.

Isihaka alisimamishwa kwa mwezi mmoja na kurejea kikosini baada ya kumaliza adhabu yake, wakati Banda ametakiwa kuandika barua ya kujieleza.

Ikumbukwe Mayanja alianza kazi Januari tu Simba akirithi mikoba ya Muingereza, Dylan Kerr aliyesitishiwa Mkataba kwa matokeo mabaya.

Chanzo: Bin Zubeiry

Haji Manara Apata Ajali Ya Barabarani
Stewart Hall Afichua Siri Ya Ushindi Dhidi Ya Warabu