Kocha mkuu wa timu ya Coastal Union ya Tanga, Ally Jangalu amesema kwamba timu yake imepoteza mechi ya wikendi iliyopita baada ya kushindwa kutumia baadhi ya nafasi walizotengeza. Coastal ilichapwa 3-0 na Mtibwa Sugar katika uwanja wa Manungu Complex, Turiani na hivyo kuendelea kubaki chini ya msimamo.

“Mchezo ulikuwa mzuri, ulikuwa wa upinzani.” anasema Jangalu ambaye timu yake itacheza na JKT Mgambo siku ya Jumatano, “Mpira ni mchezo wa makosa, tulitengeneza nafasi ambazo hatukuweza kuzitumia vizuri, na makosa yetu tuliyofanya ndiyo yamesababisha tupoteze mchezo huo”.

Magoli ya Mtibwa yalifungwa na Mdhamir Yasin 22′, Ramadhani Shija Kichuya 81′ na Ally Makalani 89.’ Mwamuzi Ngole Mwangoli kutoka mkoani Mbeya alichezesha vizuri mchezo huo.

“Sisi tumekubali matokeo, tumefanya makosa, tukafungwa goli 3 halali. Mchezo ulichezeshwa bila upendeleo, sikuona makosa ya waamuzi na kama yalikuwapo basi ni yale ya kibinadamu tu, naweza kusema wamechezesha mpira mzuri na tumekubali matokeo.”

Coastal imeendelea kubaki nafasi ya pili kutoka mkiani wakiwa na pointi 16 (alama sawa na African Sports walio mwisho wa msimamo).

“Mashabiki wetu hawapaswi kukata tamaa, tunajiandaa na mchezo ujao dhidi ya Mgambo siku yb Jumatano. Bado tuna nafasi ya kupambana na kufanya vizuri.

Florentino Perez Akalia Kuti Kavu Bernabeu
Magufuli amuapisha Balozi Kijazi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi