Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, itaendelea kesho Jumamosi Septemba 30, mwaka huu kwa michezo saba itayochezwa kwenye viwanja tofauti nchini.

Katika ligi hiyo ambayo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imeifanya tathimini ya awali na kuona kwamba inakwenda vizuri, Mechi za Jumamosi zitakuwa kati ya Young Africans na Mtibwa Sugar ya Morogoro.

Young ambayo tayari imekusanya pointi nane inachuana na kinara huyo wa Ligi Kuu ya Vodacom tangu ianze, Mtibwa Sugar ya Morogoro ambayo hadi sasa imekusanya pointi 10. Timu zote zimecheza mechi nne hadi sasa.

Mbali ya mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, mechi nyingine za kesho zitakuwa ni kati ya Ndanda itakayokuwa mwenyeji wa Lipuli FC kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara. Ndanda ina pointi nne ilihali Lipuli ina pointi tano.

Majimaji ambayo ina pointi mbili baada ya mechi nne, inaikaribisha Kagera Sugar inayoshika mkia katika msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa kupata pointi moja baada ya mechi nne. Mchezo utafanyika Uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Azam FC ambayo inafungana pointi na Mtibwa Sugar kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kesho itakuwa mgeni wa Singida United kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma. Singida United ina pointi tisa baada ya mechi nne.

Mbeya City imesafiri moja kwa moja hadi Shinyanga ambako kesho inacheza na Mwadui kwenye Uwanja wa  Mwadui. Mbeya City imekusanya pointi sita hadi sasa baada ya mechi nne ilihali wenyeji wao Mwadui hadi sasa wana pointi tatu.

Ndani ya Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Mbao FC itaikaribisha Tanzania Prisons ya Mbeya kwenye mchezo mwingine wa VPL. Rekodi zinaonesha kwamba Mbao FC hadi sasa ina pointi nne wakati Tanzania Prisons ina pointi nane.

Kule Uwanja wa Mabatini uliko Mlandizi mkoani Pwani, Ruvu Shooting FC itachuana na Njombe Mji katika mchezo mwingine wa VPL. Ikumbukwe tu kwamba hadi sasa baada ya mechi nne, timu hizo – Ruvu Shooting na Njombe Mji zote zimekusanya pointi tatu.

Keshokutwa Jumapili kutakuwa na mchezo mmoja tu wa VPL ambako Simba itakuwa mgeni wa Stand United ya Shinyanga katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Guardiola: Sergio Aguero amepata mpasuko kwenye mbavu
Halmashauri nchini zaagizwa kurudisha fedha za miradi