Shujaa wa klabu bingwa nchini Hispania FC Barcelona, Lionel Messi ametofautiana na mashabiki wake, kwa kusema hakuwahi na wala hatofikiria kujiingiza kwenye upinzani dhidi ya mshambuliaji wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo.

Messi, ambaye kwa sasa bado anaendelea kujiuguza jeraha la goti, amefikia hatua ya kuanika jambo hilo hadharani, kutokana na malumbano yanayoendelea kila kona duniani hususan kwenye mitandao ya kijamii, baina ya mashabiki wake na wale wa Cristiano Ronaldo ambao wamekua wakijadili nani ni makali zaidi ya mwenzake.

Messi amesema, yupo kwenye soka kwa lengo la kuzisaidia timu za Barcelona pamoja na Argentina na si kumtazama mtu kama wengi wanavyomuingiza kwenye zahma hiyo, ambayo kwake haina mantiki yoyote.

Amesema atakuwa mpuuzi kama akili na uwezo wake atavielekeza kwa mtu mmoja ama wawili, kutokana na kuhitaji umaarufu ama sifa za kuwa bora duniani zaidi ya wengine.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28, ameongeza kuwa hawezi kuwalazimisha mashabiki wake kukubaliana na msimamo alioutoa, lakini bado ukweli utabaki moyoni mwake kwa kuamini hashindani na yoyote zaidi ya kuzitazama Barcelona na Argentina, ambazo zinahitaji msaada wake kwa kushirikiana na wachezaji wengine.

Malumbano kati ya mashabiki wa Lionel Messi dhidi ya Cristiano Ronaldo yameibuliwa tena kwa kasi mwanzoni mwa juma hili, baada ya shirikisho la soka dunaini FIFA, kutangaza orodha ya wachezaji wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa dunia kwa mwaka 2015.

Shirikisho la soka duniani FIFA, lilitoa orodha ya wachezaji 23 ambao watachujwa na kufikia watatu na kuingia kwenye kinyang’anyiro cha tuzo ya mchezaji bora wa dunia wa mwaka huu, kwenye hafla zitakazofanyika Januari 11 mwakani, mjini Zurich nchini Uswiz.

Siku Moja Kabla Ya Kura, Wachambuzi Wa Kimataifa, Tafiti Zinatoa Ushindi Kwa Huyu…
Agnes Masogange Ang’ang’ania Licha Ya Kukataliwa