Serikali imewataka Maafisa Habari na Mawasiliano katika Wizara, Taasisi, Idara na Mamlaka za Mikoa na Wilaya nchini kutangaza mafanikio ya miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Hayo yamesemwa Mjini Morogoro na Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas wakati alipokuwa akizungumza na Maafisa Habari na Maafisa TEHAMA katika mafunzo ya uwekaji wa taarifa katika tovuti za Mikoa na Halmashauri.

Dkt. Abbas amesema Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika Mikoa na Halmashauri zake, hivyo ni wajibu wa Maafisa Habari kuhakikisha kuwa taarifa zinazowekwa katika tovuti hizo  zinaonyesha mafanikio ya Serikali katika utekelezaji wa miradi hiyo.

“Ipo miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ikiwemo miradi ya umeme vijiji, ambapo Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi hiyo, hivyo ni wajibu wa Maafisa Habari kuhakikisha kuwa taarifa za utekelezaji wa miradi inawafikia wananchi” amesema Dkt. Abbas.

Amesema kuwa Serikali ipo mbioni kuanza utaratibu wa kupima utendaji kazi wa Maafisa Habari na Mawasiliano katika Wizara, Taasisi, Idara na Mamlaka za Mikoa na Wilaya ili kuangalia ni kiasi gani wameweza kutangaza mafanikio ya Serikali katika maeneo yao ya kazi.

Aidha, ameongeza kuwa utaratibu huo wa upimaji utaweza kuainisha Wizara, Idara, Taasisi na Mamlaka za Mikoa na Wilaya zinatoa taarifa zake kwa umma, ambapo taarifa hiyo itaweza kuwasilishwa katika Mamlaka za juu Serikalini kwa ajili ya utekelezaji.

Hata hivyo, amesema kwa sasa suala la utoaji wa taarifa kwa umma si suala la utashi badala yake ni matakwa ya kisheria, hivyo Serikali inaandaa barua zitazoelezwa kwa Watendaji wakuu katika mamlaka za Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kuhusu umuhimu wa utoaji wa taarifa kwa umma.

 

Mafunzo hayo ya uwekaji wa taarifa katika tovuti yamehusisha Mikoa 5 ya Morogoro, Tanga, Simiyu, Kilimanjaro na Arusha na halmashauri zake.

Video: JPM atoa angalizo zito kwa viongozi, Chadema wapania bunge la Bajeti
Makamba ataka rasilimali za nchi zitunzwe