Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi (Saa 72) iliyokutana jana Januari 4, 2018 imejadili mechi mbalimbali za Ligi Kuu (VPL) Daraja la Kwanza (FDL) na Daraja la Pili (SDL).

LIGI DARAJA LA KWANZA

Mechi namba 37 Kundi B (JKT Mlale 1 v Mufindi United 0). Klabu ya Mufindi United imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na Kiongozi wake Hussein Turuka kutoa lugha chafu kwa Mwamuzi katika mechi hiyo iliyofanyika Desemba 31, 2017 mjini Songea. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Klabu.

Mechi namba 40 Kundi B (Mawenzi Market 1 v Polisi Dar 0). Klabu ya Mawenzi Market imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na washabiki wake kutaka kuwapiga waamuzi na kuwashawishi ball boys kuchukua mipira iliyotoka nje na kuwapelekea jukwaani.  Adhabu hiyo katika mechi hiyo iliyochezwa Desemba 31, 2017 ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Klabu.

Pia Kocha Mkuu wa Mawenzi Market amepewa Onyo Kali kwa kuchelewa kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre-macth meeting) kwa dakika saba. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi namba 39 Kundi C (Dodoma FC 3 v Alliance Schools 2). Klabu ya Alliance Schools imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa timu yake kuonyeshwa kadi zaidi ya tano katika mechi hiyo iliyofanyika Desemba 30, 2017 mjini Dodoma. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(10) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Klabu.

Mchezaji Shaban William wa Alliance Schools amesimamishwa, hadi suala lake la kumpiga Mwamuzi litakaposikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF. Uamuzi wa kumsimamisha umezingatia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Usimamizi wa Ligi.

Waamuzi wote wanne; Andrew Shamba, Abdallah Mkomwa, Athuman Athuman na Omari Juma wamefungiwa miaka mitatu kila mmoja kwa kuchezesha mechi hiyo chini ya kiwango. Adhabu dhidi ya waamuzi hao imezingatia Kanuni ya 38(1a) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.

Pia Kamishna wa mechi hiyo Mackshem T. Nzunda amefungiwa miaka mitatu kwa kushindwa kutoa taarifa ya mchezo kwa usahihi. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 39(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Kamishna.

Kamati imeomba suala la waamuzi hao ambao baadhi yao ni wa Ligi Kuu, kupitia TFF liwasilishwe kwenye chombo chenye dhamana ya kisheria ya rushwa kufanyiwa uchunguzi zaidi.

Maamuzi kamati ya uendeshaji na usimamizi wa ligi – Ligi daraja la pili
Maamuzi kamati ya uendeshaji na usimamizi wa ligi – Ligi kuu Tanzania bara